Mabeki, washambuliaji wamvuruga kocha Stand United

Muktasari:

  • Benchi la Ufundi la klabu ya Stand United limeeleza kuwa safu ya ushambuliaji na beki bado inawaumiza kichwa katika kusaka pointi tatu katika mechi za Ligi Kuu.

Mwanza. Kocha wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ amesema safu yake ya ushambuliaji na beki bado inamuumiza kichwa.

Stand United ‘Chama la Wana’ ya mjini Shinyanga hadi sasa wamekusanya pointi 22 na kukaa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 21.

Akizungumza baada baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao, Kocha Bilo alisema pamoja na kucheza soka safi vijana wake, lakini tatizo bado lipo kwa beki na washambuliaji.

Alisema mara kadhaa mabeki wamekuwa wakijichanganya na kujikuta wakifungwa mabao mepesi, huku washambuliaji nao wakikosa umakini katika kufunga mabao wanapopata nafasi.

“Wacheza vizuri ila umakini ndio mdogo kwa mabeki na washambuliaji, sisi benchi la ufundi tutazidi kuumiza vichwa kuhakikisha tunarekebisha kasoro hizo ili kupata matokeo mzuri,” alisema Billo.

Kocha huyo ambaye amekiongoza kikosi hicho tangu kipande Ligi Kuu, alisema anaamini timu hiyo itafanya vizuri na kumaliza Ligi katika nafasi nzuri.

Hata hivyo Bilo alikiri kuwa Ligi ni ngumu na timu yoyote inapofanya makosa hata kama ipo uwanja wake wa nyumbani lazima itafungwa na kueleza kuwa bado hawajakata tamaa.

“Niwaombe mashabiki na wadau wa soka waendelee kutusapoti, Ligi ni ngumu na timu ikizembea hata ikiwa nyumbani lazima ifungwe, lakini hatujakata tamaa mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti,”alisema Kocha huyo.