Mabao ya Manchester City yanamhusu Fellaini kumbe

Muktasari:

  • Fellaini alianza kama mbadala wa Pogba lakini Mourinho alisema mpango wake ni kumuingiza Fellaini kipindi cha pili ili kuvuruga mipango ya City.

London, England.MANCHESTER City ni moto wa nyika, unawaka tu, haupoi na kocha wake, Pep Guardiola amesema anafyekelea mbali yeyote anayekuja mbele yake.

Kikosi cha Manchester City kiliisambaratisha kile cha Man United katika Manchester Derby iliyopigwa pale Etihad na wenyeji City kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Lakini Kocha wa Man United, Jose Mourinho amelalamikia mipango yake ilivurugika kwa kiasi kikubwa baada ya Paul Pogba kuumia na kulazimika kumchezesha Marouane Fellaini.

Mourinho alisema kuwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa City kimeisononesha timu yake na kuifanya kuwa nyuma kwa pointi 12 nyuma ya mabingwa hao watetezi.

Pogba hakuwemo kwenye listi ya juzi na alikuwa jukwaani akiwa kwenye suti na tai akiangalia timu yake ikisulubiwa.

Fellaini alianza kama mbadala wa Pogba lakini Mourinho alisema mpango wake ni kumuingiza Fellaini kipindi cha pili ili kuvuruga mipango ya City.

Alipoulizwa kama kweli hasa kukosekana kwa Pogba kunaweza kuwa sababu ya kipigo, Mourinho alisema: “Si mimi wa kuzungumzia mchezaji ambaye hakuwepo.

“Pamoja na hayo, ukweli ni kwamba tulimmisi. Kikubwa ambacho kilituvuruga ni hili la Fellaini kuanza kwa sababu si wa kucheza dakika zote 90.

Naye alicheza lakini hana mapafu mapana ya dakika 90. Na kawaida huwa namwingiza dakika za mwishomwisho za mchezo.”

Hata hivyo, ushindi wa City ulichangiwa kwa kiasi kikubwa cha wachezaji wake kuchangamka muda wote wa mchezo.

Alikuwa Ilkay Gundogan aliyefunga bao dakika nne kabla ya filimbi ya mwisho na kuipa ushindi mnono timu hiyo.

Manchester United ilipata matumaini ya kusawazisha baada ya bao la penalti ya Anthony Martial lakini mabao yakabadilika kabisa upepo.

Hata hivyo, Mourinho alisema City ilikuwa bora zaidi kwani ilitoka kwenye ushindi wa 6-1 dhidi ya Southampton na ushindi mwingine wa mabao 6-0 dhidi ya Shakhtar Donetsk lakini yenyewe ilikuwa na matokeo ya kuungaunga dhidi ya Bournemouth na Juventus.

Pia, Mourinho alisema City ni wazi inafanikiwa kutokana na uwekezaji wake. United ndiyo timu pekee katika 10 bora iliyoruhusu mabao zaidi ya iliyofunga.Imefunga mabao 20 na kufungwa 21 katika mechi zake 12 msimu huu.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa City, Pep Guardiola alisema alijipanga kushinda mchezo huo na anafurahi wachezaji wake walitimiza maagizo yake.

Katika hatua kama hii msimu uliopita, ushindi wa Manchester City wa mabao 2-0 dhidi ya Leicester City uliifanya timu hiyo kuwa na pointi nane zaidi ya Manchester United ikiwa na mabao 33.

Liverpool ilikuwa na pointi 12 kufikia Novemba 18 na imefanya vizuri zaidi msimu huu kwa kufikisha pointi 30 japokuwa timu hiyo yenye maskani yake Anfield iko nyuma ya Manchester City kwa pointi.