Mabao ya Azam FC yampa raha Pluijm

Wednesday July 11 2018

 

By Olipa Assa, Mwananchi

Dar es Salaam. Mabao manne iliyopata Azam katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, yamemuibua kocha mpya wa kikosi hicho Mholanzi Hans van der Pluijm.

Azam juzi ilijiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame, baada ya kuilaza Rayon Sports Rwanda kwa mabao 4-2, yote yakifungwa na mshambuliaji Shabani Idd.

Pluijm aliyekaa kwenye benchi kwa mara ya kwanza kuiongoza Azam akitokea Singida United, alisema amebaini timu hiyo ina wachezaji wenye vipaji ambao wanahitaji kuongezewa mbinu za kiufundi na kuwa kikosi bora nchini.

Kocha huyo alisema alitumia mfumo wa 4-3-3 unaojumuisha mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu ambao umeonyesha matunda.

Pluijm alisema matokeo hayo yamempa morari ya kuwaongezea wachezaji mbinu za kiufundi kujiandaa na mchezo wa nusu fainali dhidi ya Gor Mahia utakaochezwa leo.

“Nimeanza kuona picha halisi namna nitakavyokuwa naandaa timu kupigania ubingwa wa Kagame na Ligi Kuu msimu ujao.

“Najua Azam iliifunga Gor Mahia katika mchezo wa fainali mwaka 2015, hii ni changamoto kwangu kupata ushindi kwa mara nyingine naamini haitakuwa kazi ndogo,”alisema Pluijm aliyewahi kuinoa Yanga.

Advertisement