Mabao kibao yametupiwa VPL

Wachezaji wa kigeni wameng’ara katika ufumaniaji nyavu kuliko wazawa kwenye Ligi Kuu Bara, huku Yanga ikiweka rekodi ya wachezaji wake wote wa kigeni kufunga isipokuwa kipa Farouk Shikhalo.

Mchezaji mmoja tu mzawa, Wazir Junior ndiye aliyewatoa kimasomaso wachezaji wa Kitanzania ndani ya kikosi hicho cha Jangwani akiwa amefunga bao.

Wakati Ligi Kuu ikiingia raundi ya tisa, tayari mabao 120 yamefungwa, huku Azam na Simba zikiongoza kwa kufunga idadi kubwa ya mabao. Timu hizo zimefunga mabao 14 kila mmoja zikifuatiwa na Yanga iliyofunga mabao 10. Katika mabao 120, 35 yamefungwa na wachezaji 18 wa kigeni wakati 84 yakipachikwa na wazawa 68.

Hii ina maana kuwa katika kila mabao matatu yaliyofungwa, moja lilifungwana na wachezaji wa kigeni.

Lakini pia kwa wastani kila mchezaji wa kigeni amefunga wastani wa mabao mawili wakati wazawa 52 walichangia bao mojamoja na 16 ndio waliofunga mawili kila mmoja. Hadi sasa kwenye chati ya ufungaji - tano bora inaongozwa na mapro watatu na wazawa wawili ambao ni Prince Dube (Azam) aliyefunga mabao sita akifuatiwa na Meddie Kagere wa Simba aliyefunga manne sawa na Obrey Chirwa (Azam), Meshack Abraham (Gwambina) na Adam Adam (JKT Tanzania).

Yanga mapro wote saba kati ya wanane walio ndani ya kikosi hicho wamefunga isipokuwa Shikhalo. Kati ya mabao 10 ambayo imefunga, tisa yamefungwa na mapro na moja likifungwa na mzawa, huku Simba na Azam nazo zikibebwa na wachezaji wa kigeni.

Mapro walioibeba Yanga ni beki Lamine Moro na kiungo Mukoko Tonombe wenye mabao mawili kila mmoja, washambuliaji Michael Sarpong, Carlos Carlinhos, Yacouba Sogne na Haruna Niyonzima na Tuilisa Kisinda waliofunga moja kila mmoja, huku Junior akiwa nalo moja. Kwa upande wa Azam, kati ya mabao 14 waliyofunga, ni mawili tu yamefungwa na wazawa Iddi Seleman ‘Nado na Ayoub Lyanga, huku 12 yakifungwa na wageni Prince Dube (6), Obrey Chirwa (4), Richard Djodi na Ally Niyonzima waliofunga moja kila mmoja.

Huko Simba katika mabao 14 waliyovuna, 11 yamefungwa na wageni na matatu na wazawa - Mzamiru Yassin (2) na John Bocco aliyeweka nyavuni bao moja.

Mapro wa Simba wanaoing’arisha ni Meddie Kagere (4), Chris Mugalu (3), Clatous Chama (2), Pascal Wawa na Luis Miquissone waliofunga bao moja moja kila mmoja.