Mabao 32 yamtibua Kocha Panama Queens

Muktasari:

Panama ilianza kupokea kichapo cha mabao 11-1 kutoka kwa Mlandizi Queens

Mwanza. Unaambiwa baada ya kushuhudia timu yake ya Panama Queens ikifungwa mabao 32 katika mechi tatu za kwanza za mzunguko wa pili, Kocha Mtwana Khamisi ameanza kukata tamaa ya kusalia Ligi Kuu ya Wanawake.

Panama ilianza kupokea kichapo cha mabao 11-1 kutoka kwa Mlandizi Queens na mtanange wa pili wakanyukwa 10-0 na Simba Queens kabla ya kukubali kichapo cha tatu cha 11-1 dhidi ya Alliance Girls Juzi Jumatatu katika Uwanja wa Nyamagana.

Akizungumza na Mwanaspoti Khamisi alisema ni ngumu kusalia Ligi Kuu kama kikosi chake kitaendelea kucheza bila kusikiliza maelekezo yake uwanjani, jambo ambalo linapelekea kuruhusu idadi kubwa ya mabao.

“Wewe mwenyewe umeona kilichokuwa kinatokea, natoa maelekezo lakini Vijana wanakwenda kufanya mengine, tupo mkiani kwenye msimamo, tukiendelea hivi tutashuka daraja, lazima tukubali kubadilika” alisema Khamisi.