Mabadiliko ligi kuu England

LONDON, ENGLAND. MABADILIKO Ligi Kuu England. Mahasimu wawili, Manchester United na Liverpool wameungana mkono kwenye mpango wa kufanya mabadiliko ya haraka kwenye Ligi Kuu England jambo litakalohusisha mkutano wa dharura wa klabu zote 20 leo Alhamisi.

Mpango huo unaofahamika kwa jina la ‘Project Big Picture’, ulifichuka Jumapili iliyopita wakati wamilikiwa klabu ya Liverpool, Fenway Sports Group (FSG) ilipothibitisha nyaraka zilizotambulika kama ‘Revitalisation’ wakiwa na mpango wa kufanya mabadiliko ya uendeeshaji wa Ligi Kuu England, kitu kilichoungwa mkopo na Man United, jambo litakalosababisha mtikisiko mkubwa kwenye ligi hiyo maarufu.

Mpango huo utafanya timu za Ligi Kuu England kupungua hadi kufikia 18, huku pesa nyingi zikipelekwa kwenye English Football League (EFL) na licha ya kwamba utaratibu huo utazipa nafuu timu za Big Six, hata hivyo imeelezwa zipo nyingine zitakazopinga mpango huo.

Wapinzani wengi wamejitokea hadharani kupinga mpango huo, ikiwamo serikali ya Uingereza, ambao wametishia kuivua mamlaka ya soka Chama cha Soka (FA) kama ikiona inazidiwa nguvu. Ripoti zinadai kwamba mmiliki wa Liverpool, John Henry na Mmarekani mwenzake, anayemiliki Man United, Joel Glazer walikuwa kwenye mazungumzo mazito Jumatatu kutafuta namna ya kupambana na mapingamizi hayo.

Matajiri hao wanataka timu mbili ziondoshwe kwenye Ligi Kuu England na kuongeza nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mpango huo wenye utata mwingi umeripotiwa kwamba utazipa nguvu zaidi klabu za Big Six, lakini ukitoa usawa kwenye mapato yatokanayo na malipo ya dili za televisheni.

Hata hivyo, hadi sasa klabu nne zinazounda hiyo Big Six bado hazijaeleza bayana kuunga mkono mpango huo.

Wakati Liverpool na Man United zikithibitishwa kuwa timu pekee zinazotaka mpango huo, timu nyingine nane zimeweka wazi kwamba haziungi mkono mpango huo.

West Ham, Brighton, Burnley, Sheffield United na Crystal Palace ni miongoni mwa timu zinazopinga mpango huo. Timu nyingine zilizobaki hazisema kitu, huku Arsenal ikishindwa kukaa upande wowote wa kukubali au kukataa.

Wamiliki hao klabu za Man United zinataka mpango huo uanze kufanyika msimu wa 2022-23. Mpango huo utatoa sapoti kubwa ya kipesa EFL hadi Pauni 700 milioni, ikiwamo Pauni 250 milioni za hasara iliyotokana na Covid-19.

Mpango huo umemshawishi mwenyekiti wa EFL, Rick Parry na yupo tayari kuunga mkono, lakini anakabiliwa na vitisho vya FA ambao wanaweza kupiga kura yao ya veto na kuzuia mabadiliko hayo.