Mabadiliko Bernabeu

Muktasari:

  • Mastaa kama Gareth Bale, Marco Asensio na Toni Kroos wametajwa ni majina machache yatakayofunguliwa mlango wa kutoka huku Los Blancos wenyewe wakiwa na dhamira ya kuwanasa Hazard na Rice kwanza baada ya kumnasa Eder Militao kutoka Porto.

MADRID, HISPANIA.ZINEDINE Zidane amekiri kwamba kutakuwa na kikosi cha kutisha sana huko Real Madrid kwa yale mapinduzi yatakayofanyika mwishoni mwa msimu huu huku Eden Hazard na Declan Rice wakiwekwa kwenye orodha.

Bosi huyo wa Los Blancos anatazamiwa kuwa na zaidi ya Pauni 400 milioni za kutumia kwenye usajili katika dirisha lijalo huku mastaa kibao waliopo kwa sasa kwenye kikosi hicho wakitarajiwa kufunguliwa mlango wa kutokea. Zidane ametua Bernabeu kuchukua mikoba ya Santiago Solari Machi mwaka huu, baada ya Muargentina huyo kuingia hapo kumbadili Julen Lopetegui mwaka jana.

Na ujio wa Zidane kwenye kikosi hicho umekuwa ukihusishwa na mipango ya kunaswa mastaa wengi wenye majina makubwa wakiwamo Wafaransa wawili, Paul Pogba na Kylian Mbappe wanaotamba kwenye vikosi vya Manchester United na Paris Saint-Germain.

Wakati kikosi chake kikijiandaa na mechi dhidi ya Leganes jana Jumatatu, Zidane alisema: “Wachezaji watu wote ni muhimu na wazuri, lakini tutakwenda kufanya mabadiliko. Hapa kuna wachezaji wengi sana wanaweza kuipatia pesa klabu. Mabadiliko yatafanyika mwisho wa msimu. Tutafahamu mabadiliko gani tutakayofanya na ni wachezaji gani tunaotaka kuwabadili.”

Mastaa kama Gareth Bale, Marco Asensio na Toni Kroos wametajwa ni majina machache yatakayofunguliwa mlango wa kutoka huku Los Blancos wenyewe wakiwa na dhamira ya kuwanasa Hazard na Rice kwanza baada ya kumnasa Eder Militao kutoka Porto.

Baada ya hapo itaanza mchakato wa kuwasajili Mbappe na Pogba huku kocha Zidane akionekana kuwa na mpango wa kumpiga bei kipa Thibaut Courtois na kubaki na chaguo lake Keylor Navas.