Maajabu ya Chelsea vs Arsenal leo

Muktasari:

Kwa maana rahisi ni kwamba Arsenal ina wachezaji wawili tu ndio wanaoweza kupata namba kwenye kikosi cha Chelsea kwa sasa. Kweli?

LONDON, ENGLAND

SI unajua leo Jumamosi kinapigwa kitu cha London derby huko Emirates wakati Arsenal watakapowakaribisha Chelsea. Basi, wachambuzi wa mambo ya soka wakatengeneza kikosi cha Kwanza kinachotokana na wachezaji wa timu hizo mbili.

Kitu cha ajabu bana, eti kikosi kizima cha Arsenal kina wachezaji wawili tu, ndio wanaopata namba kwenye timu hiyo ya pamoja.

Kwa maana rahisi ni kwamba Arsenal ina wachezaji wawili tu ndio wanaoweza kupata namba kwenye kikosi cha Chelsea kwa sasa. Kweli?

Baki na jibu lako. Timu hizo mbili zilizotofautiana pointi sita, zitamenyanan kwenye mechi hiyo wakichuana kuwamo ndani ya Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwenye kikosi hicho cha pamoja, kipa wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga, ndiye anatapata nafasi ya kuanza mbele ya makipa wawili wa Arsenal, Bernd Leno na Petr Cech.

Kwenye safu ya ulinzi, si Laurent Koscielny, Shkodran Mustafi wala Sokratis Papastathopoulos waliopata nafasi na ukuta wa timu hiyo wote unaundwa na wakali wa Chelsea, ambao ni David Luiz na Antonio Rudiger wakicheza kati na Marcos Alonso na Cesar Azpilicueta wakiwa pembeni na kuwaweka benchi mabeki wa pembeni wa Arsenal kama Sead Kolasinac, Nacho Monreal na Hector Bellerin.

Kwenye kiungo hakuna cha Granit Xhaka wala Lucas Torreira, eneo hilo limetawaliwa na mastaa wa Chelsea, ambao Jorginho na N’Golo Kante ili kufanya mfumo wa kiuchezaji wa 4-2-3-1 kufanya vyema. Wachezaji wa Arsenal sasa hao wawili, wanaingia kwenye sehemu ya ushambuliaji, ambapo Pierre-Emerick Aubameyang akikaa upande wa kushoto kwenye mstari wa washambuliaji watatu wanaocheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambaye ni Alexandre Lacazette. Kwenye kikosi hicho, Eden Hazard atacheza nyuma ya mshambuliaji wa kati na kulia ni Mbrazili Willian.

Jambo hilo litawafanya wachezaji wengine kama Pedro, Aaron Ramsey na Alex Iwobi kusubiri kwenye benchi, wakati kipaji kama Mesut Ozil haijulikani kama hata benchi atakuwapo kutokana na kiwango chake cha siku za karibuni.