MZOZO anakufa maskini katikati ya utajiri wa soka

Friday September 7 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD NA OLIPA ASSA

HUENDA ni wadau wachache wa soka ndio wasiomjua Heri Chibakasa a.k.a Heri Mzozo, ila asilimia kubwa wanamjua hadi watoto wadogo.
Unajua kwa nini? Jamaa amekuwa na mchango mkubwa kwenye soka la Tanzania hasa katika kuibua vipaji na kuvisaidia kupata mafanikio makubwa nchini.
Kwa miaka zaidi ya 24 amekuwa akiifanya kazi ya kuwaibua na kuwasafishia njia nyota mbalimbali wanaotamba kwa sasa ndani na nje ya nchi, huku mwenyewe akiishia maisha ya kawaida sana licha ya kuwa katikati ya utajiri.
Kuanzia kina Shekhan Rashid, Athuman Idd Machupa mpaka hawa kina Salum Abubakar 'Suber Boy', Jabir Aziz Stima na Mohammed Hussein 'Tshabalala' jamaa kahusika katika kuwatengenezea maisha. Kwanini asiwe tajiri? Mbona kina Mino Raiola au Mendes wanaodili na uwakala wa wachezaji wananuka harufu ya ankara?
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na mvumbua vipaji huyo aliyeiasisi klabu ya Friends Rangers iliyopo kwa sasa Ligi Daraja la Kwanza na kuwa kama kisima cha kuzalisha nyota wanaotamba kwa sasa ndani na nje ya nchi kisoka.

MZOZO NI NANI?
Huyu jamaa bwana ni kati ya wadau wachache wenye mchango mkubwa katika soka la Tanzania, kwani amewaibuka nyota wengi na amejikita katika kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 20.
Alianza kama utani kwa kuiasisi klabu ya Friends Rangers mwaka 1994, yenye maskani yake pale Magomeni Kagera, jijini Dar es Salaam.
Klabu hiyo inatumia Uwanja wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere, zamani Makurumla kama uwanja wake wa mazoezi kwa miaka mingi na kuibuka nyota mbalimbali tangu wakati huo akiwa kama kocha wa klabu hiyo ya Daraja la Kwanza.
Mzozo ana historia ya aina yake iliyojaa simanzi, furaha kidogo, huku mengi yakiwa yametawala zaidi na wachezaji alioanza nao safari baada ya mafanikio na kuamua kumkimbia na kumwacha akiendelea kupambana na hali yake.

UHALISIA WA MAISHA YAKE
Historia ya maisha yake imejaa hisia kali za maumivu, hasa pale anapoweka wazi kwamba kuna wakati anajuta kutumia muda mwingi kwenye soka ambalo halijampa mafanikio yoyote licha ya wachezaji waliopitia mikononi mwake kuishi kifahari.
"Sina mafanikio niliyopata kupitia soka, mpaka sasa nyumba yangu imefika katikati sijaimaliza kutokana na kukosa pesa, lakini niliowapigania wanaishi katika majumba ya kifahari.
"Pesa ninayopata najikuta siwezi kuwaacha wale nilionao kwa sasa, kwani wanahitaji kufika mbali, soka nalichukulia kama wito kama wanavyofanya mapadri na mashehe wanaosubiri kulipwa na Mungu ndivyo ilivyo kwangu, japo soka kwa sasa ni biashara kubwa duniani.
"Hii inatokana na wachezaji kutokuwa na elimu ya soka ikiwemo viongozi wa klabu kutoangalia aua kufikiria wanawatoa wachezaji hao katika mikono ya nani, kiukweli hii kazi imenitia umaskini wa hali ya juu, laiti ningekuwa nimeingia nao mikataba ningekuwa tajiri mkubwa hapa Tanzania.
"Kwa sasa nimebadilisha utaratibu wachezaji ambao nawachukua sasa nitaingia nao mikataba ila wale wa zamani nitaendelea kuishi nao kijamaa maana ndio maisha nilioanza nao, siwezi kuwabadilikia kama wanavyofanya wao wanapokuwa wamepiga hatua.
"Nina vijana wengi sasa hivi tena wana uwezo mkubwa, mikataba nitakayoingia nayo itaanzia kwa wazazi wao ili watambue ni jinsi gani natumia muda na kupoteza pesa nyingi kuwasaidia vijana wao ambao baadaye hawawi na msaada wowote, hivyo nitashirikisha wazazi wao kusaini hiyo mikataba kwa utaratibu unapaswa kufuatwa," alisema Mzozo.

AMEVUNA Sh 4 MILIONI TU
Mzozo amewatoa kisoka wachezaji wengi, lakini baadhi yao ni wachezaji watatu ndiyo wanajua thamani ya mchango wa Mzozo kwenye maisha yao ya soka na kumpa chochote katika mafanikio yao japo si makubwa.
Nyota hao ni Jabri Aziz 'Stima' ambaye aliwahi kumpa Sh 500,000 aliposajiliwa Simba, Fred Cosmas Lewis alipotua Prisons na Mbeya City kwa nyakati tofauti alimpa jumla ya Sh 1 milioni na Joseph Mahundi aliposaini Azam FC alimpatia Sh 1 milioni.
"Hao ni wachezaji waliokumbuka kunipa chochote katika pesa zao za usajili, sikuwaomba wala kuwabughudhi ni wao waliona warudishe kama shukrani kwa kile nilichowafanyia, hata nilipochukua pesa hizo nilizipeleka zisaidie timu," anaeleza.

MSUVA HADI KINA TSHABALALA
Simon Msuva, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Salum Abubakar 'Sure Boy' na Said Ndemla ni baadhi ya wachezaji waliopita mikononi mwake na sasa wana mafanikio makubwa kwenye soka. Mzozo anaeleza juu ya wachezaji hao
"Mchezaji kama Msuva, huyo nilimchukua kwenye timu ya Wakati Ujao kwa makubaliano maalumu, nilimbadilisha nafasi alikuwa anacheza mshambuliaji wa kati nikamwambia kwa umbo lake anapaswa kucheza winga za pembeni na muda wote anatakiwa kukimbia na mipira ndipo atawini na imekuwa hivyo.
"Nilifanya kazi kubwa kuhakikisha anaonekana, nilienda naye Azam FC kwenye timu ya vijana mwaka 2009 na niliwaambia viongozi wampe mkataba lakini hawakuwa na jicho la kuona kipaji hicho, ndipo akatolewa kwa mkopo Moro United ambako alionekana na Yanga.
"Ajabu katika mikataba yake sijui chochote, labda wenzangu wa Wakati Ujao wanahusishwa na hilo, lakini ndio hivyo maisha yanaendelea, ila amekuwa mchezaji ambaye ananipigia simu na tunashauriana mambo mbalimbali ya maisha ya mpira.
"Kuna siku alinitafuta tulipoonana alinipa Sh100,000, sikumuomba hii inaonyesha kwamba ni mchezaji anayethamini mchango wa watu ambao wamefanya ndoto yake itimie.
"Mchezaji mwingine ambaye alikuwa mpita njia lakini anakumbuka kurudi kusapoti timu ni Ndemla na hivi karibuni kanunua mipira miwili ya timu na huwa anatoa michango ya hapa na pale, tofauti na mastaa ambao wamefanikiwa kucheza nje na hakuna wanachokifanya," anasema.
Kuhusu kiungo wa Azam FC, Sure Boy anasema licha ya kumtoa mbali, lakini hakuwahi kuambulia chochote kwenye mikataba yake, isipokuwa anatoa michango ya timu pindi anapohitajika kufanya hivyo.
"Mchezaji kama Tshabalala licha ya kutumia muda mwingi kuhakikisha anafikia ndoto zake, ila sijawahi kupata chochote kwake na sina maana haniheshimu la, ana nidhamu ila kimaslahi ndio hivyo na nimeacha kama ilivyo ili mengine yaendelee.
"Nilitumia muda mwingi sana kuwalea hao vijana kwa kuishi nao maana kitanda alichokuwa analala Sure Boy ndicho alilalia Tshabalala baada ya Sure Boy kufanikiwa kuichezea Azam. Waliishi pale kwa Mzee Ntare ambaye sasa ni marehemu.
"Ishu ya Tshabalala tangu aanze kucheza Kagera Sugar ilinipa changamoto kubwa sana na baba yake ambaye hakujua hata mtoto analala wapi ila niliishi nao kwa upendo mkubwa.
"Yote yamepita na ni changamoto za soka la Bongo kwani sio hao tu wapo kama kina Rashid Mandawa nao ndivyo hivyo hivyo sina nilichokipata kwake hata ile mwenyewe kukumbuka thamani yangu haipo, siwezi kuwaomba ila wanatakiwa kujitambua."

ANAISHI  WAPI?
Mzozo anasema alipanga nyumba yenye vyumba vinne, maeneo ya Magomeni Kagera alikokuwa akikaa na wachezaji, lakini kwa sasa ameamua kujiengua na kurudi kwenye nyumba ya familia.
"Nimerudi nyumbani, yaani naishi kwenye nyumba ya familia ipo hapa hapa Magomeni, ile niliyokuwa nimepanga sijarudisha nimewaacha wachezaji wanakaa humo maana bado naendelea kuwa nao, sijaoa ila nina kijana wangu anaitwa Sabri ana miaka 25 ameoa na ana watoto wawili.
Alipoulizwa yeye mpango wa kuoa umekaaje! Alijibu "Nitaoa mpaka nitakapomaliza nyumba yangu, ingawa sijui nitamaliza lini, lakini pia huyo mwanamke awe tayari kwenda kuishi na mimi kijijini Ifakara.
"Nina mpango wa kwenda Ifakara kwa ajili ya kilimo kwani nina ekari 14 na mpango wangu ni kujikita katika kilimo tu, maana hakuna faida yoyote ninayoipata kwenye soka. Natafuta pesa ili ninunue ng'ombe wanne na majembe mawili maalumu kwa ajili ya kilimo, sasa sijui hawa wanawake wa mjini kama atakubali kwenda kuishi maisha ya kijijini na kulima."

HUU NDIO MWISHO KISOKA
Ana vijana zaidi ya 60 anaowasimamia katika soka, wote wanamuangalia yeye na wengine wanasoma ambapo pia anatoa mchango wa kuwalipia ada na mmoja wa wachezaji anataka kumpeleka Chuo cha Biashara (CBE).
"Sitaacha kuwasimamia ila nitaacha ule mfumo wa ujamaa sasa ni kusainishana mikataba, nitafanya vyote kwa pamoja kilimo na mpira maana mambo yangu mengi hayajafanyika kutokana na kuendekeza ujamaa kwani mtu kama mimi ningekuwa mbali sana kupitia mpira, yaani ungekuwa umenilipa kama ningefuata taratibu za kimikataba, sasa sina wa kumlaumu.

BADO ANALIPWA  AZAM FC
Mzozo ni miongoni mwa watu ambao wameipa mafanikio makubwa Azam FC tangu ikiwa inapigana kupanda Ligi Kuu Bara. Mzozo aliisaidia Azam kutwaa ubingwa wa Kombe la Uhai akiwa na nyota wake kama Himid Mao, John Bocco, Sure Boy na wengine.
Aliondoka Azam baada ya mfumo wa uongozi kubalika lakini bado klabu hiyo inathamini mchango wake na ndiyo maana alipoondoka alizawadiwa gari aina ya Toyota Baloon.
Lakini pia hadi sasa Azam humsaidia Mzozo kifedha kuendesha maisha yake ambapo yeye anafafanua; "Kiukweli nawashukuru sana Azam FC wameona kazi yangu na wananipa mshahara kila mwisho wa mwezi ambao unaendesha maisha yangu na sio kwamba wameniajiri katika klabu yao hapana. 
"Si hivyo tu bali nilinunuliwa na gari aina Baloon, baada ya kufundisha timu yao ya vijana ilitoa wachezaji kibao kama Farid Mussa, Himid na wengineo. Hivyo maisha yanaenda kwa juhudi zangu.
"Similiki nyumba, lakini nina magari mawili, hilo nililopewa na Azam na lingine aina ya Crown lenye thamani ya Sh 20 milioni ambalo nilizawadiwa na dada mmoja anaitwa Mamu baada ya kumsaidia mawazo ya hapa na pale kimaisha, alipofanikiwa akarudi na zawadi hiyo, huyu dada nilimfahamu kupitia kwa rafiki yangu ila anajua thamani na utu wa mtu,"anasema.

NIA YA KUANZISHA TIMU
Anasimulia kwamba wakati anaanzisha Friends Rangers mwaka 1994, nia yake hasa ilikuwa ni kuinua vipaji vya wachezaji na kuhakikisha wanafikia ndoto zao, anakiri hilo limefanikiwa kwa asilimia 80, ila shida inakuja pale wanapovunja ujamaa na kubadili maisha tofauti na yale walioanza nayo.
Kosa kubwa analokiri kufanya ni kwa wachezaji alioanza nao, anadai hakuweza kuingia nao mikataba ya kuwataka wanapopata timu ndani na nje waweze kurudisha gharama za malezi aliyoyatoa kwao.
"Malengo yangu yametimia asilimia 80 ila ninatamani sana siku moja kutwaa ubingwa ili Manzese kutoke timu ya ligi kuu na wadau watambue mimi sio mkorofi ila nimejariwa sauti kali, hivyo wasije wakadhani tutakuwa wababe lah,"anasema.

KUFUNGUA KAMPUNI
"Nitakuwa na kampuni yangu binafsi ambayo itakuwa inasimamia wachezaji, kila kitu kitakwenda kisheria, soka la sasa umebadilika na ni biashara kubwa duniani, hivyo wachezaji watambue hilo wale wote watakaopita kwangu kuanzia hivi sasa watakuwa chini ya mikataba na zama za ujamaa zimekwisha.
"Timu zitakazochukua wachezaji kupitia mikono yangu nazo zijiandae kuingia makubaliano ya kulipana kila mchezaji anapoongeza mkataba ama kumsajili, mfumo huu utakuwa kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta na Simba ambapo alienda TP Mazembe waliilipa Simba hata alipoenda KR Genk hiyo ni kwa sababu walimlea."
MWISHO

Advertisement