MTU WA PWANI : Kutoka kwa Samatta, Msuva hadi kwa Ng’anzi

Muktasari:

  • Tofauti na zamani, leo hii ni rahisi kwa timu ya DR Congo kumsajili mchezaji wa Kitanzania kwa sababu Samatta alishaacha alama hapo ambayo inawafanya thamani ya wachezaji wetu kule DR Congo iwe juu.

AKIWA na umri mdogo wa miaka 19 tu, Mbwana Samatta aliondoka zake Tanzania na kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga na miamba ya soka nchini humo, TP Mazembe.

Kilichofuata baada ya hapo ni historia tamu ambayo itadumu milele ndani ya nchi hiyo kutokana na kile ambacho Samatta alikifanya ndani ya kikosi cha Mazembe, ambayo ni moja ya klabu zilizofanikiwa zaidi barani Afrika ikitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano na lile la Shirikisho la Afrika mara mbili.

Akiwa na Mazembe, Samatta alipata tuzo ya mchezaji bora Afrika anayecheza ndani ya Afrika, aliwahi kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa ligi ya mabingwa Afrika mara mbili, ameshakuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu huko DR Congo lakini pia alishinda taji la ubingwa wa ncghi hiyo mara kadhaa.

Inawezekana mafanikio hayo yakaonekana ni ya Samatta binafsi lakini kwa upande mwingine yamekuwa na neema kwa taifa letu kwa sababu ni chachu ya kulitambulisha soka la Tanzania huko DR Congo.

Tofauti na zamani, leo hii ni rahisi kwa timu ya DR Congo kumsajili mchezaji wa Kitanzania kwa sababu Samatta alishaacha alama hapo ambayo inawafanya thamani ya wachezaji wetu kule DR Congo iwe juu.

Unapoona TP Mazembe leo wanahaha kumnasa kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib, ni matunda ya kazi nzuri iliyofanywa kwenye klabu yao na Samatta ambaye sasa hivi amekamilisha kibarua kingine cha kuitangaza na kufungua milango kwa wenzake huko Ubelgiji anakotamba kwenye klabu ya KRC Genk.

Wakati Samatta akifanikiwa kuacha alama kule DR Congo na sasa akipambana kule Ubelgiji, mshambuliaji mwingine wa Ktanzania, Saimon Msuva sasa hivi anawatesa kweli Waarabu kule Morocco.

Tangu aliposajiliwa akitokea Yanga, mwaka 2017 amekuwa na urafiki mkubwa na nyavu kwenye mechi mbalimbali za mashindano nhini Morocco akichezea Difaa El Jadida na msimu uliomalizika ambao ni wa pili kwake alimaliza akiwa nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu nchini humo lakini ndiye mfungaji bora wa klabu yake msimu wa 2018/2019.

Kama ilivyokuwa kwa Samatta, mabao ambayo Msuva anaendelea kupachika kule Morocco yanazidi kulitambulisha soka la Tanzania nchini humo na yanasafisha nia kwa wachezaji wa Kitanzania kuwa bidhaa hadimu kwa timu za huko siku za usoni.

Kama Msuva angefanya vibaya kule basi milango kwa wachezaji wa Kitanzania kwenda kucheza soka la kulipwa Morocco ingekuwa migumu kufunguka lakini bahati iliyoje, mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa Yanga hajawaangusha wenzake kutokana na kazi aliyoifanya.

Maana yake kutokana na juhudi za Samatta na Msuva, sasa ni rahisi kwa nyota wa Kitanzania kwenda kucheza soka la kulipwa huko Ubelgiji, DR Congo na hata Morocco.

Njia hii imekuwa ikitumiwa zaidi na wachezaji wa mataifa ya Afrika Magharibi ambao kadri wanavyopata nafasi ya kwenda mahala fulani kucheza soka la kulipwa, wao ndio wanakuwa chachu ya kufungua milango kwa wenzao kwa kuoneyesha viwango bora ambacho vinavyoleta ushawishi kwa timu za mahali walikokwenda kutazama na kunasa nyota wengine kutoka nchi zao.

Ni jambo ambalo linapaswa kuigwa na kila mchezaji wa Kitanzania anayepata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kadri watakavyokuwa wakifanya vyema ndivyo milango itazidi kufunguka kwa wenzao wengine kuingia katika nchi ambazo wao wapo kwa ajili ya kusaka malisho mazuri na nafasi ya kupiga hatua zaidi.

Kwa bahati nzuri, inavyoonekana sumu ya Samatta inaanza kusambaa taratibu kwa wachezaji wengine kutoka hapa nchini ambao wanapata fursa ya kuchjeza soka la kulipwa nje ya nchi kwani wengi wao wanafanya vizuri.

Mfano mzuri wa hilo tunauona kwa kinda wa timu ya taifa ya vijana chni ya umri wa miaka 20 ‘Kilimanjaro Stars’, Ally Ng’anzi ambaye anazidi kutamba katika Ligi Daraja la Kwanza kule Marekani.

Alitoka Singida United na kujiunga na MFK Vyskov ya kule Czech ambako alifanya vizuri na kunaswa na Forward Madison ya Marekani.

Kile alichokifanya ndani ya Czech kimepelekea kusajiliwa kwa Mtanzania mwenzake, John Tiber ambaye alikuwa naye kwenye kikosi cha Singida United. Tiba kama utani vile alipita Singida United akiwa na malengo ya kufika mbali na sasa safari yake inaendelea na mafanikio yameanza.

Muda mfupi tu baada ya kutua Marekani ameanza kuwa mchezaji tegemeo na staa wa Minnesota United iliyomchukua kwa mkopo kutoka Forward Madison.

Baada ya kufungua milango kule Czech, inaonekana wazi anakwenda kufanya hivyo Marekani. Ni ishara ya kupokelewa vyema kwa darasa la Samatta na Msuva.