MTU WA PWANI : Jadida, Mazembe wanatukumbusha udhaifu wetu

Muktasari:

Singano amesajiliwa na Mazembe kwa mkataba wa miaka mitano na dau la usajili alilopata linatajwa kufikia Dola 50,000 (Sh115 milioni).

SIKU moja baada ya Azam FC kutangaza kuachana na kiungo mshambuliaji wake, Tafadzwa Kutinyu ambaye ni raia wa Zimbabwe, Horoya FC ya Guinea ilitangaza kumnasa mchezaji huyo aliyewahi kuichezea pia Singida United.

Kimafanikio na historia, Horoya ni klabu kubwa Afrika kuliko Azam FC, Simba na Yanga.

Imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Washindi Afrika mwaka 1978, lakini pia imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo - mwaka 2018 na msimu wa 2018/2019.

Hata kwa maana ya uwekezaji na kiuchumi, hakuna timu ya Tanzania inayoigusa Horoya.

Kwa kulidhihirisha hilo, miezi kadhaa iliyopita ilitoa kitita cha Dola 100,000 kumnasa aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo, suala ambalo huwa gumu kwa klabu zetu kutoa donge nono kama hilo kuvunja mkataba wa mchezaji wa timu nyingine.

Siku kadhaa baadaye, Horoya hiyohiyo ilifanya usajili wa kushangaza kwa kumnyakua winga Enock Atta Agyei ambaye alitupiwa virago na Azam FC ambayo ilionekana kutoridhishwa na kiwango chake.

Katika hali ya kushangaza, nyota huyo wa Ghana kama ilivyokuwa kwa Kutinyu naye alitangazwa kuachwa na Azam siku moja nyuma.

Ni Azam hiyohiyo ambayo ilishuhudia Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye waliachana kwa makubaliano binafsi akijiunga na vigogo vya soka Afrika, TP Mazembe.

Singano amesajiliwa na Mazembe kwa mkataba wa miaka mitano na dau la usajili alilopata linatajwa kufikia Dola 50,000 (Sh115 milioni).

Hali kama hiyo haijaikuta Azam FC peke yake, bali hata Simba ambayo wakati ikiwa kwenye mipango ya kuachana na kiungo James Kotei kutoka Ghana, ghafla alitua kwenye klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Nani asiyejua ukubwa na mafanikio ya Kaizer Chiefs mbele ya timu kama Yanga, Simba na Azam FC.

Inawezekana vipi mchezaji asiyefaa Simba akafaa kwa matajiri hao wa Afrika Kusini ambao wako chini ya bilionea Kaizer Motaung.

Inawezekana vipi klabu zetu zikawa na ubora kiasi hicho hadi zikaona wachezaji hawafai, lakini timu ambazo ni kubwa na zenye mafanikio zaidi yao zikaamua kuwaona wachezaji hawana maana na kuamua kuwatosa?

Inavyoonekana kuna tatizo fulani katika soka letu ambalo linasababisha klabu zetu kuwapoteza wachezaji wazuri ambao upande mwingine huonekana kuwa lulu.

Inawezekana tatizo hilo ni klabu zetu kushindwa kulinda ubora wa wachezaji wetu kwa kutowapa huduma stahiki ambazo zimesababisha viwango vyao viporomoke au kuonekana viko chini au vinakosa watu wa kushindwa kung’amua namna gani timu itamtumia mchezaji ili awe na mchango siku za usoni.

Lakini kingine inaonekana klabu zetu zinafanya maamuzi kwa utashi wa kishabiki na hisia binafsi na si vigezo vya kiufundi, jambo linalofanya ziwaache wachezaji ambao bado wana ubora wa kuzitumikia na kuzisaidia.

Na tatizo lingine ambalo pengine linachangia hilo ni makocha wa klabu zetu kutokuwa na utayari na uthubutu wa kuwatumia wachezaji kwa utashi wa kiufundi na badala yake kupanga vikosi kwa shinikizo kutoka kwa viongozi.

Usajili wa mchezaji kama Nickson Kibabage ambao umefanywa na Difaa El Jadida ya Morocco hivi karibuni unaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kutupa tafakuri juu ya namna mabenchi ya ufundi ya timu zetu yanavyotoa uamuzi wa kiufundi.

Kibabage ambaye alikuwa nyota wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, kilichoshiriki Fainali za Afrika kule Gabon mwaka 2017, hakuwa anapata nafasi kwenye kikosi cha wakubwa cha Mtibwa Sugar na hata alipotolewa kwa mkopo Njombe Mji nako hakuwa anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, Jadida imeng’amua kipaji chake na kuamua kumsajili huku ikimpandisha kwenye kikosi cha wakubwa moja kwa moja ambacho ameanza kufanya nacho mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.

Ina maana Mtibwa na Njombe Mji zina ubora na mafanikio makubwa kuliko Jadida hadi zikaona Kibabage hastahili kuchezea vikosi vyao vya kwanza?

Kama taifa kuna mahali tunakosea na ni vyema tukaparekebisha, vinginevyo timu zetu zitaendelea kupoteza wachezaji wazuri kwa maamuzi yasiyo na tija ambayo yanafanywa na watu wachache.

Na hili likizingatiwa, basi tujiandae kuwa na klabu bora zinazolinda vipaji vinavyochipukia.