MTU WA PWANI : Genk wametusaidia kwa Kelvin, klabu zijitafakari

Muktasari:

Kelvin anakwenda kwenye klabu ambayo ina miundombinu na mazingira bora ya kumfanya ajengeke na kuwa mchezaji wa daraja la juu na staa mkubwa wa soka duniani kama ambavyo imefanya kwa baadhi ya nyota waliowahi kupita hapo mfano nyota wa Manchester City, Kevin De Bruyne.

KELVIN John ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali huko Uganda ambako kwa kuongoza chati ya ufungaji bora wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 20.

Akiwa ndani ya jezi ya Timu ya Taifa ya Tanzania Bara kwa vijana wenye umri kama huo ‘Ngorongoro Heroes’, tayari kinda huyo mwenye umri wa miaka 17 ameshapachika mabao saba (7).

Kasi ya kufumania nyavu ambayo Kelvin John anayo wala sio jambo la kushangaza. Ana kipaji cha kufunga na amekuwa akifumania nyavu kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Alianzia kwenye mashindano ya kirafiki kwa nchi za Afrika Mashariki 100 na Kati, wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 tu kisha akatamba kwenye mashindano ya Afrika Mashariki kwa vijana wa umri kama huo na kisha akaonyesha ubora wake kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana wa umri kama huo yaliyofanyika hapa nchini mwezi Aprili.

Sehemu zote ambazo kinda huyo amekuwa akienda kufanya majaribio kwa ajili ya kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa amekuwa hasiti kucheka na nyavu.

Haikushangaza kuona klabu kama HB Koge ya Denmark, Ajax ya Uholanzi, Manchester City ya England na KRC Genk ya Ubelgiji zikiisaka saini yake mara baada ya kumfuatilia kwa ukaribu kupitia mikanda 100 ya video, mechi alizocheza pamoja na majaribio aliyofanya kwenye baadhi ya timu barani Ulaya.

Hata hivyo, ni Genk ambayo taarifa za uhakika zilizothibitishwa na mchezaji mwenyewe zimefafanua kuwa imeshamalizana naye na pindi atakapofikisha umri wa miaka 18 atajiunga nayo rasmi kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa.

Kwa kundi kubwa la wadau na wapenzi wa mchezo wa soka nchini, suala la Kelvin John kujiunga na Genk ni jambo kubwa na lililosubiriwa kwa hamu kwani linatoa mwanga mzuri wa muendelezo bora wa kipaji cha mshambuliaji huyo.

Kelvin anakwenda kwenye klabu ambayo ina miundombinu na mazingira bora ya kumfanya ajengeke na kuwa mchezaji wa daraja la juu na staa mkubwa wa soka duniani kama ambavyo imefanya kwa baadhi ya nyota waliowahi kupita hapo mfano nyota wa Manchester City, Kevin De Bruyne.

Baada ya kufungua milango ya mafanikio kwa Mbwana Samatta ambaye anang’aa barani Ulaya kwa sasa, kitendo cha kumnasa Kelvin John ni ishara nyingine nzuri ya namna klabu hiyo imeamua kuliweka soka la Tanzania kwenye ramani ya ulimwengu.

Pamoja na faida ambayo taifa litapata kupitia usajili wa kijana huyo, kwa upande mwingine Genk imeamua kutuonyesha udhaifu wetu ambao ni changamoto tunazopaswa kuzikalia chini na kuzifanyia kazi.

Usajili wa kinda huyo umeonyesha udhaifu wa klabu zetu kutotilia mkazo na kutotoa kipaumbele uwekezaji kwenye soka la vijana kama ambavyo misingi ya weledi kwenye soka (professionalism) inalazimisha hivyo.

Klabu zetu zimepoteza fursa muhimu ya kupata fedha kupitia usajili huo wa Kelvin John na badala yake kituo kinachomsimamia ndicho kitanufaika kwa sababu hazijaona faida ya kuwa na timu bora na imara za vijana.

Kwa nchi ambazo zinafahamu umuhimu wa kuwekeza kwenye soka la vijana, leo hii klabu mojawapo ya klabu yake ingekuwa na uhakika wa kuvuna kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa Genk kwa kumuuza mshambuliaji huyo.

Kwa kipaji alichonacho, leo hii Kelvin John alipaswa kuwa tayari anachezea kwenye kikosi cha vijana cha moja ya klabu zinazoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara lakini mwisho wa siku hilo limekuwa kinyume.

Haijawezekana kwa sababu klabu zetu hazijaamua kuwa na mfumo mzuri wa kusaka na kulewa wachezaji wenye vipaji na wanaoonyesha mwanga wa kuwa mastaa wakubwa siku za usoni (promising players).

Zingekuwa na utayari wa hilo, zingeweza kumnasa kinda huyo kupitia mashindano ya soka kwa shule za msingi Tanzania (Umishumta) ambayo ndiko kituo kinachomlea kilimuona na kumnasa mshambuliaji huyo.

Lakini pia mbali na kunufaika kibiashara, pia klabu zetu zinakosa fursa ya kuwa na wachezaji wazuri vijana walio wazawa ambao wanaweza kuzisaidia kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kwa klabu zenye uwekezaji imara katika soka la vijana, leo hii Kelvin John angekuwa staa mkubwa na muhimu kwenye kikosi kimojawapo cha timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini hayo yote yameshindwa kufanyika kwa sababu klabu zetu hazijawa na utayari wa kulipa kipaumbele soka la vijana. Kila siku viongozi wanaongea tu suala hilo lakini utekelezaji hakuna.