MTAISOMA! Klopp awaambia wapinzani ubingwa wa msimu ujao

Muktasari:

Kocha huyo Mjerumani alisema Liverpool yake itakuwa na nafasi kubwa ya kutamba msimu ujao kwenye mbio za kufukuzia ubingwa ukilinganisha na wapinzani wake kwenye mbio hizo, Manchester City.

Liverpool, England. MPO? Jurgen Klopp amewaambia wapinzani wake, wataisoma namba msimu ujao kutokana na ratiba kuwakaba huku mambo yake yakiwa mepesi.

Kocha huyo Mjerumani alisema Liverpool yake itakuwa na nafasi kubwa ya kutamba msimu ujao kwenye mbio za kufukuzia ubingwa ukilinganisha na wapinzani wake kwenye mbio hizo, Manchester City.

Huo ndio mtazamo wa Jurgen Klopp, ambaye amedai kwamba atawapa wachezaji wake muda mwingi wa kupumzika kujiandaa kwa msimu mpya, licha ya kutokuwa na ufahamu ligi ya msimu ujao itaanza lini.

Hata hivyo, Klopp alikiri kuweka mipango kwa sasa ni kujiweka kwenye wakati mgumu tu, kwa sababu klabu nyingine zitaendelea kupambana kwenye michuano ya Ulaya hadi mwishoni mwa Agosti.

Manchester City, Manchester United, Wolves na Chelsea zote zitahusika kwenye michuano hiyo ya Ulaya, ambapo kama watafika kwenye hatua za fainali, basi jambo hilo litawasogeza hadi karibu ya Septemba, ambapo kwa wakati huo, wachezaji wa Liverpool ambao, hawatakuwa na michuano yoyote baada ya Ligi Kuu England kumalizika, watakuwa na muda wa kupumzika.

Kutokana na hilo, Klopp amewaonya wapinzani wake kwamba wataisoma namba kwenye mbio za ubingwa msimu ujao.

Alisema: “Wachezaji watakuwa na muda mchache wa kupumzika, tutakuwa na kipindi kifupi pia cha kujiandaa na msimu mpya kulingana na lini msimu mpya utaanza na hilo linazihusu timu ambazo bado zipo kwenye michuano ya Ulaya.

“Sijui watakabiliana vipi na hilo. Kama Man City watakwenda hadi fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hiyo itakuwa mwishoni mwa Agosti, ni ngumu kwao. Au kwa Man United, Chelsea na Wolves.

Wote bado wapo kwenye michuano ya Ulaya na hakika watakuwa kwenye wakati mgumu.”

Liverpool ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Atletico Madrid, kitu ambacho Klopp anaamini kimekuwa na faida kubwa kwa upande wake kutokana na hali iliyotokea kwa sasa.

Kwa timu ambazo bado zipo kwenye michuano ya Ulaya, hiyo ina maana kwamba wachezaji wao watakuwa na muda mfupi sana wa mapumziko, licha ya Klopp kudai kwamba hafahamu msimu mpya wa ligi utaanza lini.

“Acha tusubiri, kwa sababu lazima kuwepo na mipango ya pre-season na kusubiri watu wapange ligi inaanza ligi. Kwa upande wetu itakuwa ngumu, lakini uzuri ni kwamba hatuwezi kuanza kitu chochote hadi timu nyingine zimalize mechi zao, nadhani itakuwa Septemba huko, kabla ya kufahamu msimu unaanza ligi.

“Kwa kipindi hiki, sisi tutatumia kupumzika.”

Klabu pia katika kuelekea msimu mpya zitakuwa kwenye ukata mkubwa wa kiuchumi kwa sababu hata zile mechi za pre-season ambazo zilikuwa zikiwaingizia pesa nyingi kutokana na viingilio, hali itakuwa tofauti kwa sababu mashabiki hawatahusika kutokana na kukomesha maambukizi ya virusi vya corona.

Wakati huo huo, mabosi wa Ligi Kuu England wameripotiwa kwamba leo, Alhamisi wataanza mjadala wa kuhusu ni lini msimu wa 2020/21 unapaswa kuanza, huku kukiwa na tarehe mbili mezani, Agosti 29 na Septemba 12. Suala la kufunguliwa kwa dirisha la usajili liliripotiwa litajadiliwa katika kikao kijacho cha mabosi hao wa Ligi Kuu England.

Kuhusu Liverpool, ambaye usiku wa jana Jumatano ilitarajia kuwakabili Brighton ugenini, imeshajibebea ubingwa wa Ligi Kuu England, hivyo watacheza mechi zao kukamilisha ratiba tu, wakipata nafasi ya kupumzisha mastaa wao wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya msimu ujao.

Miamba hiyo ya Anfield haipo kwenye michuano yoyote, ikitupwa nje kwenye Kombe la Liga, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa wa England, Man City, Man United, Chelsea na Arsenal bado zinashiriki. Pia, klabu hizo zimekuwa kwenye harakati za kuboresha vikosi vyao.