MRS MAJIZZO: Hapana chezea penzi wewe

Friday November 23 2018

 

By Rhobi Chacha

MUITE Mrs Majizo sio Elizabeth Michael tena ama Lulu kama ambavyo amezoeleka kwa muda mrefu tangu anaingia kwenye gemu ya Bongo Movie.

Ndio! Kwa wale waliokuwa wakisubiri kusikia vigelegele na wale waliojiandaa kwenda kuupiga ubwabwa, muda ndio umekaribia kwani, Lulu na mchumba wake Francis Shiza a.k.a Majizo, mambo ndio yamezidi kunoga.

Baada ya Lulu kuvishana pete ya uchumba na Majizzo, usiku wa Septemba 30, mwaka huu, hatimaye wawili hawa wamepiga hatua nyingine na sasa wanakaribia kabisa kuanza maisha mapya.

Wakati walimwengu wakianza kutokwa povu wakijadili hatua hiyo, ghafla Jumapili iliyopita Majizzo na Lulu wakasogea tena hatua nyingine mbele ikiwa ni takribani siku tano tu baada ya msanii huyo wa Bongo Movie kumaliza kutumia kifungo chake.

Lulu alihukumiwa kifungo chake kwa kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua bila kukusudia mpenzi wake, Steven Kanumba.

Baada ya tukio hilo, Lulu akaingia kwenye ukurasa wake wa Instagram, akaweka emoji ya ishara ya kushukuru na kuandika: “Deal Done”.

Tukio hilo limeufanya uhusiano wa wawili hawa kuwa gumzo kwelikweli huko kwenye mitandao ya kijamii huku wenyewe wakionekana kupatwa mzuka zaidi kwa hatua wanayoikaribia.

Mwanaspoti limezungumza na Lulu, ambapo amesema upendo anaonyeshwa na Majizo ni wa kipekee licha ya kupitia vipindi vigumu kwenye maisha.

“Toka nimekuwa na Majizzo amekuwa ananipa upendo kama baba na tumepitia wakati mgumu sana katika uhusiano wetu, hivyo hadi kufikia hatua hii ni jambo la kumshukuru Mungu na kuzidi kusali kila kukicha,” alisema Lulu.

Hata hivyo, kama ulikuwa hufahamu ni kwamba Lulu na Majizzo kwa sasa wamefikisha miaka minne ya uhusiano wao, ambapo penzi lao lilianza kuchipua mwaka 2014.

Lakini, tofauti na wengine penzi la Lulu na Majizo, ambaye ni mzazi mwenzie na mrembo Hamisa Mobeto, lililoanza kwa siri kuwa na kila wakati walipokuwa wakihojiwa na vyombo vya habari walikuwa wakikana.

Hata hivyo, lilikuja kushika kasi zaidi baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba, Majizo na Mobetto hawapo kwenye mahusiano mazuri na hapo ndipo kazi ya kupigana vijembe na kutemeana shombo kwenye mitandao ya kijamii ikashika kasi.

 

Mapito yake

Lulu ni mmoja wa mastaa waliopitia mapito ya misukosuko katika mapenzi na Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yamemfanya kuwa jasiri.

Ukiangali kwa umri alionao Lulu amepitia mambo makubwa zaidi ya uwezo na akili yake ikiwemo kesi ya mauaji ya Kanumba ambayo ilikuwa gumzo huku magwji wa sheria wakipambana kutetea vifungu kutokana na umri wake.

Aprili 7, 2012, Lulu aliibua mshtuko baada ya kudaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia huku pia ikidaiwa kwamba, walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na ugomvi huo umetokana na wivu.

Mwaka 2014 baada ya kuanzisha uhusiano wa mapenzi na Majizo uliingia kwenye mzozo mkali, lakini baadaye uliimarika tena mwaka mmoja baadaye.

Lulu akiwa kwenye umri mdogo, iliibuka skendo akidaiwa kuwa ni mjauzito huku mhusika ikidaiwa kuwa ameingia mitini.

Hata hivyo, Lulu aliwahi kulieleza Mwanaspoti kwamba: “Kama hizi mimba za kuambiwa zingekuwa kweli, basi ningeshakuwa na watoto hata saba. Sina mimba kama unavyoniona na wala sijawahi beba mimba.”

 

Lulu ni nani?

Akiwa na umri wa miaka saba tu, kipaji chake cha kuigiza kilionwa na msanii nyota na ambaye, ni mmoja ya watu wanaoheshimiwa sana na Lulu, Dk. Cheni kupitia bonanza la kuibua vipaji. Wakati huo Dk. Cheni alikuwa akitamba kwenye Kundi la Kaole hivyo, kumvuta Lulu kwenye kundi hilo na nyota yake ikaanza kung’ara fasta na kukubalika kwa mashabiki.

Lulu alionyesha uwezo mkubwa na kuvaa uhalisia na nafasi anazopewa kuigiza, jambo ambalo lilimtengenezea mashabiki wengi.

 

Advertisement