MO aongoza kikao cha kwanza Bodi ya Wakurugenzi Simba

Muktasari:

Klabu ya Simba ilifanya uchaguzi wake mkuu Novemba 4, na kupata viongozi watakaoiongoza timu hiyo kwa miaka minne ijayo.

 

Dar es Salaam. Mwekezaji mtarajiwa wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ leo amefanya kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo.

MO Dewji amekutana na viongozi hao ikiwa ni wiki moja baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo jijini Dar es Salaam.

Mo Dewji aliongoza kikao hicho kilichohudhuria na  Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, Mwenyekiti Swedi Mkwabi na wajumbe, Dk Zawadi Kadunda, Seleman Haroub, Hussein Kitta, Asha Baraka na Mwina Kaduguda waliochaguliwa wiki iliyopita.

Wengine ni kaimu Rais wa zamani wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again', wajumbe Said Tulliy, Musley Al- Ruwey na Mlamu Nghambi.

Hata hivyo uongozi wa Simba ulitoa picha za wajumbe na Mo kukutana katika mitandao yake ya jamii  bila ya kutoa taarifa yoyote juu ya mkutano huo wa leo.

Viongozi hao wamekutana ikiwa ni siku moja baada ya Shirikisho la Soka Africa (CAF), kutangaza ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kupangwa dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Katika ratiba hiyo, wawakilishi hao wa Tanzania wataanza kwa kukipiga na Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa kwanza ambao Simba itaanzia nyumbani.

Mbabane inakumbukwa baada ya kuitupa nje Azam FC katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika katika raundi ya kwanza mapema mwaka 2017.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mchezo michezo ya kwanza itachezwa kati ya Novemba 27 na 28 na baada ya hapo itacheza mchezo wa marudiano ugenini kati ya Desemba 4 na 5 mwaka huu.

Mshindi wa jumla wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Nkana Red Devils ya Zambia na UD Do Songo ya Msumbiji ili kusaka timu itakayofuzu hatua ya makundi.

Katika mashindano hayo pia JKU ya Zanzibar itaanzia nyumbani itakapoivaa Al Hilal ya Sudan na mshindi wa jumla wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mechi baina ya APR ya Rwanda na Club Africain ya Tunisia.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Mtibwa Sugar imepangwa kukutana na Northern Dynamo ya Shelisheli na mshindi wa mechi hiyo atacheza na KCCA ya Uganda wakati Zimamoto ya Zanzibar itaanza na Kaizer Chief ya Afrika Kusini na ikishinda mchezo huo itakutana na mshindi wa mechi kati ya El Geco ya Madagascar na Deportivo Unidado ya Guinea ya Ikweta.

 

Wadau wanena

Kocha wa zamani wa Pan African, Kagera Sugar na timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 ‘Ngongoro Heroes’, Adolph Rishard alisema Simba wanatakiwa kujipanga kwani mechi hiyo sio rahisi.

“Ukiangalia Mbabane Swallows siku hizi wanacheza sana soka la ushindani haitakuwa rahisi kuitoa, Simba ijiandae vizuri kwani,” alisema Rishard.

Naye beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Simba inatakiwa kuingia katika mchezo huo na mingine itakayofuata kwa kuwaheshimu wapinzani na kuhakikisha inamaliza mechi zote kwenye uwanja wake wa nyumbani.

“Mbabane ni timu ya muda mrefu na imeimarika zaidi kutokana na kushiriki mashindano hayo mara nyingi hivyo lazima Simba waiheshimu ili wapate matokeo mazuri.

Alisema Simba inapaswa kuweka mikakati hasa kuhakikisha wanashinda mabao mengi katika mchezo wa nyumbani kwa sababu mchezo wa marudiano wanaweza kupata ugumu kama ilivyokuwa kwa Azam,” alisema Pawasa.

Naye Kocha zamani wa timu ya Taifa Stars, Dk Mshindo Msola, alisema Simba inatakiwa kujiandaa vizuri kwani mechi za kimataifa sio kama za Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Ingawa Simba inafanya vizuri katika Ligi ya hapa nyumbani, kwa mtazamo wangu Hii inatokana na timu nyingi wanazokutana nazo katika ligi yetu ni dhaifu kutokana na hali halisi ya kiuchumi.

Wajipange vizuri na wasiidharau timu yoyote kwani mashindano ya kimataifa ni tofauti na ligi yetu, ingawa Simba ina kikosi kizuri lakini wanatakiwa wasijiamini sana bali wajipange,” alisema.

Iwapo Simba ikifanikiwa kuitoa Mbabane Swallows, inaweza kujikuta ikiangukia kwa kigongo kingine kati ya timu ya UD Songo ya Msumbiji au Nkana Red Devils ya Zambia, ambazo zote zimekuwa zikifanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka huu timu hiyo ya Msumbiji ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako iliishika nafasi ya 3 kwenye kundi B ikiwa na pointi tatu, ikifunga mabao matano na kufungwa kumi.

 

Tofauti yake na Simba

Katika msimamo wa Ligi ya Swaziland, iko nafasi ya nne ikiwa imecheza michezo minane kushinda mitano sare moja na kupoteza miwili, imefunga mabao 10 imefungwa saba, ipo pointi nane nyuma ya vinara Green Mamba FC.

Ina washambuliaji wanne kikosini Sabelo Ndzinisa,27, Sandile Hlatjwako,30, Simanga Shongwe 28 wote raia wa Swaziland na mshambuliaji kinda Daniel Atakorah 21, mzaliwa wa Nigeria.