VIDEO: MO ainogesha Simba ya Afrika

Muktasari:

  • Ushindi wa Simba umekuja siku moja baada ya Mtibwa Sugar kupata ushindi wa 4-0 dhidi ya Northen Dynamo ya Shelisheli na kuifanya Tanzania kuwa na mtaji wa mabao nane katika michuano ya Afrika ya 2018-2019.

SIMBA jana Jumatano iliwapa furaha mashabiki wake baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini, huku bilionea wao, Mohamed ‘MO’ Dewji aliyeonekana kwa mara ya kwanza uwanjani tangu alipotekwa Oktoba 11 na kupatikana siku tisa baadaye akinogesha ushindi huo wa kishindo.

Mashabiki wa Simba walilipuka baada ya kumuona hasa alipowasalimia, kuonyesha namna gani walikuwa na hamu ya kumuona na utamu ulizidi baada ya nyota wa timu hiyo kuwapa ushindi mnono.

Kama kuna watu walionuna jana basi ni mashabiki wachache wa Yanga ambao walijitokeza Uwanja wa Taifa katika mchezo huo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mashabiki hao walioshangilia kwa nguvu bao la kusawazisha la Mbabane waliumbuka na kuondoka taifa kimya kimya baada ya mabao mawili ya mapema ya nahodha John Bocco na yale ya Meddie Kagere na Cletus Chama kuwatuliza. Ushindi wa Simba umekuja siku moja baada ya Mtibwa Sugar kupata ushindi wa 4-0 dhidi ya Northen Dynamo ya Shelisheli na kuifanya Tanzania kuwa na mtaji wa mabao nane katika michuano ya Afrika ya 2018-2019.

MECHI ILIVYOKUWA

Simba ikirejea kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2013 na kung’olewa kwa aibu na Recreativo do Libolo ya Angola walioifumua mabao 5-0.

Bocco akiwa kwenye kiwango cha juu aliandika bao la kwanza dakika ya 8 kabla ya beki Guevane Nzambe kuisawazisha Mbabane bao dakika ya 23 kwa shuti kali la mbali lililomshinda nguvu kipa Aishi Manula.

Bocco aliandika bao lake la tano la michuano ya CAF akiwa na Simba kwa mkwaju wa penalti dakika ya 33 baada ya Emmanuel Okwi kuchezewa madhambi na kuifanya Simba iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1.

Mabadiliko ya Kocha, Patrick Aussems alimtoa Okwi na kumuingiza Shiza Kichuya yaliisaidia Simba kupata bao la tatu lililofungwa na Kagere baada ya kipa wa Mbabane kuteleza wakati akituliza pasi ya kurudishiwa na mwenzake na straika huyo matata wa Simba kuwahi na kufunga kiulaini dakika ya 84.

Mbelgiji aliyemuanzisha, Nicholas Gyan bila kutarajiwa katika mchezo huo, alimtoa Bocco na kumuingiza, Hassan Dilunga dakika za lala salama na kiungo huyo kutoa pasi tamu iliyomalizwa kiufundi na Chama aliyewahadaa mabeki wa Mbabane kabla ya kufumua shuti.

Hata hivyo Simba inapaswa kujilaumu kwa kukosa mabao mengi katika mchezo huo, huku wapinzani wao walionyesha sio timu nyepesi kwa kucheza soka la kufunguka licha ya kucheza ugenini, ikiwa haiijui vyema Simba.

KIFYAGIO KILA KONA

Matokeo ya Simba yamewaibua wachambuzi wa soka, Alex Kashasha na Ally Mayay walioipa asilimia 60 kwa Simba kufuzu kucheza raundi ya kwanza.

“Tafsiri ya matokeo ya leo (jana) ni kwamba Simba ipo salama kwa mchezo wa marudiano, lakini wasifikirie kwenda kupaki basi Eswatini,,” alisema Mayay. Mayay alisema wapinzani wao wanajua kuutumia vema uwanja wa nyumbani, hivyo Simba itakapowafuata kwa mechi ya marudiano Jumanne ijayo iende na falsafa ya kushambulia mwanzo mwisho ili kuwadhibiri wapinzani wao.

Mwalimu Kashasha alisema, Simba imecheza mpira mwingi, lakini wanachotakiwa ni kusahau matokeo na kuifuata Mbabane kana kwamba wao ndiyo amefungwa.

“Kocha awafanye wachezaji waone safari yao bado, watakapoifuta Mbabane wacheze kwa maelekezo, wapinzani wao sio wabaya ni timu bora japo walikuja na nadharia ya kujilinda zaidi, walipanga kushambulia kwa kushtukiza, walikuwa wazuri kutokea pembeni,” alisema.

Aliongeza mabadiliko aliyoyafanya kocha yaliisaidia Simba huku akipongeza bao la Kagere akisema limedhihirisha ukomavu wake kwenye soka.

“Hakutarajia kipa atateleza lakini uenda aliwaza inawezekana litatokea lolote ndiyo sababu hakukata tamaa na fikra zake zikawa kweli. Katika mchezo huo, Simba ilipiga mashuti tisa yaliyolenga goli huku wapinzani wao wakipiga matatu na mashuti 12 ambayo hayakulenga goli huku wapinzani wao wakipiga manne na kona tatu, Simba ilipata kona 10.