MO aibuka upya Simba

Monday September 10 2018

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Kiungo fundi wa Simba, Mohammed Ibrahim 'MO Ibrahim' ni kama amezaliwa upya kikosini humo chini ya usimamizi wa kocha Mbelgiji Patrick Aussems.
MO alisajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar miaka miwili iliyopita akacheza soka safi mwanzo lakini baadaye akashindwa kutamba na yakaibuka mambo ya sintofahamu huku akidaiwa kujiunga kwa watani wao Yanga.
Lakini, baadaye akasaini tena Simba mkataba wa miaka miwili ambao utamalizika mwishni mwa msimu ujao.
MO alishindwa kucheza katika kikosi cha kocha aliyeondoka Mfaransa Pierre Lechantre kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya utovu wa nidhamu.
Lakini, tangu Aussems atue, MO amekuwa akibadirika kila siku na kucheza kwa kiwango cha juu jambo lililomfanya Mbelgiji huyo aanze kumwamini.
Amekuwa akipewa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mazoezini na hata katika mechi za majaribio ukiwemo ule wa waliowafunga timu yao ya vijana chini ya miaka 20 mabao 4-0.
Alianzishwa pia, katika mechi yao na AFC Leopards ya Kenya ambayo pia ilikuwa ya kirafiki, wakaibuka na ushindi wa mabao 4-2.
Mechi hizo zote, amecheza kwa kiwango cha juu na mbali na kucheza nafasi hiyo ya kiungo, amefunga bao moja katika mchezo na AFC Leopards.
Huo ni mwanzo mzuri kwa MO ambaye katika kipindi cha Lechantre alipotea kabisa na hata kwenye benchi la wachezaji wa akiba kumwona ilikuwa nadra.

Advertisement