MO Dewji ampa shavu jipya Mbeligiji Simba

Muktasari:

  • Aussems aliwekewa kipengele cha kuiwezesha timu hiyo kuwa mabingwa na kufika hatua ya makundi katika Ligi ya mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameangukia neema baada ya Mwenyekiti ya bodi wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji kuweka wazi bado wanamuhitaji katika kikosi chao kwaajili ya msimu ujao.

Aussems alisaini mkataba wa mwaka mmoja na alikuwa akitajwa kutoongezewa mkataba wa kuendelea kuifundisha timu hiyo, lakini Dewji amezima mzizi wa fitna kwa kuweka wazi hatma ya suala hilo.

Dewji alisema wamefurahishwa na mwenendo wa kocha huyo na watamuongezea mkataba wa kuendelea kukifundisha kikosi chao baada ya kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu, pia kufika katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Aussems ametimiza mahitaji yetu yote ambayo tulikuwa tukiyahitaji, kwahiyo wiki ijayo tutakaa naye chini na kuona namna ambavyo tunaweza kumuongezea mkataba mpya baada ya kufanya yale tuliyokuwa tukiyahitaji," alisema.

Dewji aliongeza kocha huyo aliwaomba wamuongezee mwalimu mwingine wa viungo ili wachezaji wanapokuwa wanapata majeraha wasichelewe kurejea uwanjani.

"Mwalimu amehitaji mtaalamu mwingine wa viungo atakayesaidiana na aliyepo ili kuhakikisha wachezaji wetu wanakuwa wanapata programu nzuri zaidi pindi wanapokuwa wamepata majeraha," alisema Mo Dewji.