MIKONO YA DHAHABU LIGI KUU ENGLAND

Friday October 12 2018

 

LONDON, ENGLAND, MASHABIKI wa Ligi Kuu England hawana namna zaidi ya kusubiri kwa wiki mbili zijazo kufurahia tena utamu wa soka la klabu pale timu zao zitakashuka viwanjani kwenye mchamchaka huo.
Ile paap ni Manchester United na Chelsea na hapo ndipo mambo yanaponoga zaidi. Jose Mourinho atajiokoa kwenye kibarua chake huko Man United au mambo yatazidi kuwa mabaya zaidi huko Old Trafford. Wiki hizi mbili kutakuwa na mechi za kimataifa.
Msimu huu, Ligi Kuu England imekuwa na utamu wake kutokana na timu tatu kukabana koo kwenye kilele cha ligi hiyo, wote wakiwa na pointi 20 na kutofautiana tu tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Timu hizo zilizokabana kileleni ni Manchester City, Chelsea na Liverpool. Lakini, hilo sio mpango wetu wa leo, hapa tunataka kuwatazama makipa mahiri zaidi waliowahi kutokea kwenye ligi hiyo. Kwa takwimu tu, kuna makipa saba tu, ndio waliofanikiwa kubeba tuzo ya kipa bora wa mwaka yani, Glovu za Dhahabu kwenye Ligi Kuu England tangu zilipoanzishwa mwaka 2004.

7.David De Gea- Tuzo 1
Kipa wa Manchester United, David De Gea hatimaye alifanikiwa kubeba tuzo ya kipa bora wa mwaka kwenye Ligi Kuu England katika msimu wa 2017/18 wakati alipokuwa golini kwenye mechi 18 za ligi hiyo bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa. Ilikuwa mara yake ya kwanza kwa Mhispaniola huyo kushinda tuzo hiyo ya Glovu za Dhahabu kwenye ligi hiyo tangu alipotua Old Trafford mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid. De Gea ameingia kwenye orodha ya makipa saba waliowahi kunyakua tuzo hiyo ya makipa bora kwenye Ligi Kuu England tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004. Ni kipa wa pili pia wa Man United kufanya hivyo baada ya Edwin van der Sar. Hakika De Gea ni mwamba imara kwenye goli la Man United, asipokuwepo golini basi hata mashabiki wa timu hiyo wamekuwa kwenye mashaka makubwa.

6.Thibaut Courtois- Tuzo 1
Thibaut Courtois kwa sasa ameshaondoka kwenye Ligi Kuu England na anakipiga huko kwenye La Liga akiwa na kikosi cha Real Madrid baada ya kusajiliwa kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Kipa huyo wa zamani wa Chelsea, Courtois alibeba tuzo hiyo ya kipa bora ya kwenye Ligi Kuu England katika msimu wa 2016/17, ambao alikaa golini kwenye mechi 16 bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa huku akiisaidia Chelsea kubeba ubingwa wa ligi chini ya kocha Mtaliano Antonio Conte. Kwa sasa yupo na Los Blancos na mambo yake si mazuri, wakati huko alikotoka Chelsea wamekuwa moto chini ya Mtaliano mwingine, Maurizio Sarri.

5.Wojciech Szczesny- Tuzo 1
Kipa wa zamani wa Arsenal, Wojciech Szczesny alibeba tuzo ya kipa bora wa mwaka kwenye Ligi Kuu England katika msimu wa 2013.14. Kipa huyo wa kimataifa wa Poland hakudumu sana kwenye kikosi cha Arsenal, lakini ukweli alifannya vyema kwenye kikosi hicho kilichokuwa chini ya Arsene Wenger na kufanikiwa kunyakua tuzo hiyo ya Glovu za Dhahabu. Msimu huo, Woj alidaka mechi 16 bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa na kufanikiwa kuwapiku Petr Cech na Joe Hart kwenye kinyang'anyiro cha tuzo hiyo. Amekuwa kipa mwenye bahati sana baada ya kwenda kumrithi mkongwe Gianluigi Buffon huko kwenye kikosi cha Juventus.

4.Edwin van der Sar- Tuzo 1
Kipa wa zamani wa Manchester United, Edwin van der Sar amestaafu akiwa na tuzo moja ya kipa bora kwenye Ligi Kuu England. Mdachi huyo alibeba tuzo hiyo inayofahamika kama Glovu za Dhahabu kwenye msimu wa 2008/09 wakati alipoisaidia Man United kubeba ubingwa wa ligi huku yeye akikaa golini kwenye mechi 21 bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa. Kiwango cha Mdachi huyo kilikuwa matata kabisa kwa sababu msimu mmoja kabla aliisaidia timu yake kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwachapa Chelsea kwenye fainali iliyofanyika Moscow, Russia. Van der Sar anabaki kuwa mmoja wa makipa mahiri kabisa waliowahi kutokea kwenye kikosi hicho cha Man United chenye maskani yake Old Trafford.

3.Pepe Reina- Tuzo 3
Gwiji wa Liverpool, Pepe Reina amebeba tuzo tatu za kuwa kipa bora kwenye Ligi Kuu England. Mhispaniola huyo alibeba tuzo hizo wakati alipokuwa akitoa huduma yake kwenye kikosi cha Liverpool huko Anfield. Kwenye awamu hizo ambazo Reina alibeba tuzo za Glovu za Dhahabu kwenye Ligi Kuu England, alicheza mechi 20, 19, na 18 bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa na ilikuwa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2005 hadi msimu wa 2007/08.  Kwa sasa anacheza soka lake kwenye Serie A akikitumikia kikosi cha AC Milan. Reina aliondoka kwenye kikosi cha Liverpool baada ya kutibuana na kocha Brendan Rodgers, ambaye naye aliondoshwa na Jurgen Klopp kuja kuchukua mikoba ya kuwanoa wababe hao wa Anfield.

2.Joe Hart- Tuzo 4
Kipa Mwingereza, Joe Hart ni mmoja kati ya wakali matata kabisa kwenye Ligi Kuu England akibeba tuzo nne za ubora wa makipa kwenye ligi hiyo, Glovu za Dhahabu. Mzuiaji huyo wa mashuti, amebeba tuzo hizo zote nne za ubora alipokuwa na kikosi cha Manchester City. Alishinda kwenye msimu wa 2010/11 baada ya kucheza mechi 18 za ligi hiyo bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa.
Alibeba tena kwenye msimu wa 2011/12, akicheza mechi 17 bila ya kuokota mipira kwenye wavu wake na msimu wa 2012/13 aliocheza mechi 18 bila ya kufungwa bao na kwenye msimu wa 2014/15, ambao alicheza mechi 14 bila ya kufungwa. Kwenye dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi mwaka huu, Hart alijiunga na Burnley na anaonekana kufanya vyema huko.

1.Petr Cech- Tuzo 4
Kipa wa Arsenal, Petr Cech amenyakua mara nne tuzo ya Glovu za Dhahabu zinazotolewa kwa makipa bora wa msimu kwenye Ligi Kuu England. Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2004. Kwa kifupi tu, Cech ndio alikuwa kipa wa kwanza kubeba tuzi hiyo baada ya kuanzishwa tu. Aliisaidia Chelsea kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Englandn walipokuwa chini ya kocha Jose Mourinho msimu 2004/05, ambao alicheza mechi 24 bila ya kuruhusu mpira kutinga kwenye nyavu zake. Hadi sasa idadi hiyo ya mechi bado ni rekodi. Akashinda tena tuzo hiyo 2009/10 kwa kucheza mechi 17 bila ya kuruhusu bao, 2013/14 mechi 16 bila ya kuruhusu bao na katika msimu wa 2015/16, ambao alicheza mechi 16 bila ya kufungwa kwenye ligi hiyo, safari hii akiwa na jezi za Arsenal. Cech anashikilia rekodi ya nyakati zote ya kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao kwenye Ligi Kuu England.

Advertisement