Winga Namungo awashitua Mbeya City

WINGA wa Namungo FC, Sixtus Sabilo amesema wanatakiwa kujipanga kuikabili Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu raundi ya nne ambayo itachezwa Septemba 25 mwaka huu Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

 Namungu inaingia uwanja kucheza na Mbeya City ikiwa imetoka kupoteza dhidi ya Prisons wakati wenyeji wao wenyewe wamepoteza mechi zote tatu walizocheza ugenini na nyumbani.

 Namungo wao walishinda dhidi ya Coastal Union huku wakipoteza mbele ya Polisi Tanzania wakati Mbeya City wao walifungwa Yanga, KMC na Azam FC.

 Sabilo ameiambia Mwanaspoti Online kuwa wanahitaji umakini mkubwa kwenye mchezo huo kwani wapinzani wao wataingia kwa hasira kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri kwenye zao zilizopita.

 Amesema ni pambano ambalo litakuwa gumu hasa kwao kitu ambacho wanatakiwa kuingia kwa tahadhari kubwa ili kupata ushindi ambao utawapa nguvu ya kupambana kwenye ligi.

 “Ni mechi ngumu, hasa kwetu kwani Mbeya City wataingia wakiwa wametukamia sana ili kupata ushindi kitu ambacho tunatakiwa kujipanga kuwakabili kwenye huu mchezo,”

 "Tunahitaji sana ushindi kwani tumecheza mechi tatu ambazo tumeshinda moja tu na zote tumepoteza kitu ambapo tunatakiwa kukomaa ili kupata ushindi," amesema Sabilo

 Winga huyo amesema msimu huu ligi imeanza kuwa ngumu kitu ambacho kwao wanatakiwa kupambana ili waweze kwenda na kasi yake kwani bila hivyo watajikuta wapo nafasi mbaya kwenye msimamo.