MAONI YA MHARIRI: Taifa Stars safi ila kazi bado mbichi

Muktasari:

  • Ushindi wa mabao 2-0 iliyopata timu ya Taifa Starss dhidi ya Cape Verde  kimefufua hai tumaini ya Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Afcon tangu  tulipocheza 1980.
  • Ni takribani miaka 38 tanguTanzania imekuwa ikisubiri kuona kwa mara nyingine nchi yao inaenda katika fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika.

USHINDI wa mabao 2-0 iliyopata timu yetu ya taifa ya soka, Taifa Stras dhidi ya Cape Verde sio tu umelipa kisasi cha kipigo cha mabao 3-0, lakini pia kimefufua hai tumaini la Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Afcon tangu  tulipocheza 1980.
Kwa miaka 38 Tanzania imekuwa ikisubiri kuona kwa mara nyingine nchi yao inaenda katika fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika, hivyo ushindi wa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ni kama umeleta faraja kwa mashaviki wa soka nchini.
Wengi wanaamini na kuwa na tumaini la kuiona Stars ikiwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki fainali za mwakani zitakazofanyika nchini Cameroon, ikitoka Kundi L linaloongozwa na Uganda The Cranes ambayo imetanguliza mguu mmoja Afcon 2019.
Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo hususani soka, tunaipongeza Stars kwa ushindi huo na kulipongeza benchi la ufundi la timu hiyo kwa kufanya mabadiliko makubwa kwa aina ya mbinu za uchezaji kulinganisha na ilivyocheza mjini Praia.
Kama tulivyotoa rai mara baada ya mechi ya ugenini kwamba hatupaswi kukata tamaa na msako wa tiketi ya Cameroon, ndivyo tunavyotoa rai nyingine tena kwa sasa kwa vijana wetu kuelekea mechi mbili za mwisho zilizosalia kabla ya Stars kujua hatma yao.
Katika mechi zilizosalia, ikiwamo ile ya ugenini dhidi ya Lesotho itakayopchezwa mwezi ujao kabla ya kuisubiri Uganda katika mchezo wa mwisho utakaochezwa Machi mwakani ambayo itaamua kama Stars itaenda Cameroon ama la!
Wachezaji wa Stars pamoja na makocha sambamba na mabosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mashabiki kwa ujumla wasibweteke kwa ushindi huo na kuamini kazi imeshamalizika kwa sababu tu, Stars imepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo.
Ni kweli ushindi huo umefufua tumaini, lakini kazi bado na tunatahadharisha yale ya mwaka 2007 yasije yakatutokea tena, baada ya kuamini kuwa tiketi ya kwenda Fainali za Afcon 2008 tulikuwa nayo na kunyang'anywa tonge mdomoni na Msumbiji.
Tanzania enzi za Marcio Maximo baada ya kuifunga Burkina Faso nje ndani na kutoka sare na Senegal na kuibana Msumbiji kwao, wengi waliamini Stars ingeenda katika Fainali za Afcon 2008 zilizokuwa zifanyike Ghana.
Kiburi zaidi kilikolezwa na ushindi wa 1-0 mjini Ouagadougou, bao la Erasto Nyoni dakika ya 77 liliifanya nchi nzima kurindima kwa furaha, huku wanasiasa wakiona nafasi ya kujitafutia ujiko kabla ya kualikwa Bungeni kwa heshima zote.
Mechi ya mwisho ilikuwa dhidi ya Msumbiji tuliotoka nao suluhu kwao katika mechi ya kwanza na Stars ilikuwa na alama 8, sawa na Senegal na Msumbiji walikuwa nyuma yetu na alama sao sita. Kila shabiki aliamini Stars ilikuwa inaenda kufanya maajabu katika mchezo huo muhimu na tukawa tunasubiri kuona uwiano wa mabao ndio uamue kati yetu na Senegal nani wa kwenda Ghana.
Kilichotokea Uwanja wa Taifa, kila mtu anakumbuka! Stars ililala bao 1-0 la Ticotico na Senegal wakiwa kwao wakainyoosha Burkina Faso kwa mbaoa 5-1 na kukata tiketi hiyo ya Ghana.
Hali kama hiyo imetukutana tena mwaka huu katika Kundi L ndio maana tunawakumbusha wachezaji, makocha na hata viongozi wa TFF na mashabiki kuwa, kazi bado tunapaswa kuungana na kushikamana kwa hali na mali ili Stars ikashinde Maseru dhidi ya wenyeji wao Lesotho inayoburuza mkia katika kundi lao.
Matokeo yoyote kinyume na hapo ni kuikwamisha safari ya Stars kwani mchezo dhidi ya Uganda mwakani kwa yakini huenda ukawa wa kukamilisha ratiba tu kama hatutaweza kuchangamka ugenini.
Hivyo wakati tukiwapongeza Stara kwa ushindi dhidi ya Cape Verde, lakini pia tuweka akilini kuwa, tuna kazi ndefu mbele yetu kuliko tulipotoka na hii ilichangiwa na kushindwa kuzitumia vyema mechi zilizopita hasa mchezo wa awali dhidi ya Lesotho.
Iwapo tutaamini ushindi wa juzi umemaliza kazi, basi tujiandae tu kukutana na simanzi kama ilivyotukuta Septemba 8, 2007 pale bao la dakika nane la Ticotico lilivyonyakua tiketi ya kwenda Ghana na kuonekana sherehe zote za ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso zilikuwa bure.
Mwanaspoti linaamini Tanzaia safari hii ina nafasi ya kwenda Afcon 2019 na kuzima unyonge wa miaka 38, lakini sio kazi rahisi kama wengi wanavyofikiria kama hatutakuwa na mipango mikakati kwa mechi mbili zilizosalia ili yetu yanyooke.
Tukianza kupiga hesabu za vidole kuwa, Uganda itaifunga Cape Verde na sisi tunaenda kuwanyoosha Lesotho kwao kwa hisia tu tu bila kujipanga kuanzia wachezaji hadi maandalizi ya timu kwa mechi hiyo ya Novemba, tunaweza kuumbuka tena. Tusikubali!