MAKALA... Pep apigwa

Muktasari:

Kama hiyo haitoshi, Ancelloti ambaye wakati kitabu hiki kikiandikwa alikuwa akiinoa Bayern Munich na sasa ni kocha wa Napoli anaongeza kuhusu Ronaldo.

TOLEO lililopita tuliona jinsi Mwandishi, Luca Caioli alivyomnukuu kocha wa zamani wa Barcelona (kwa sasa anainoa Man City), Pep Guardiola ambaye alisema haamini kama atatokea mchezaji wa kumzidi Messi. Sasa endelea…

Pep Guardiola kwa upande wake aliamua kuwa wazi zaidi akisisitiza kwamba Leo (Messi) ni mwanasoka bora katika historia.

“Hakutakuwa na mchezaji kama yeye na sidhani kama atatokea mwingine kama Messi,’’ hiyo ndiyo kauli ya Pep Gurdiola, kocha aliyewahi kumuongoza Messi akiwa Barcelona kabla ya kuhamia Bayern Munich na sasa anaifundisha Man City.

Pia, kuna wale ambao hawataki kujiingiza katika mjadala huu, hawa hawataki kuwa upande wowote.

“Wote ni wachezaji wa kiwango cha juu,’’ anasema kocha wa zamani wa Ureno, Paulo Bento. “Kama wangekuwa hawachezi katika nchi moja kusingekuwa na mjadala wa nani zaidi ya mwenzake.

Mbali na hao kuna wale ambao ni mashabiki kindakindaki wa Ronaldo ambao huwaambia kitu kwa mchezaji huyo.

“Ni mchezaji aliyekamilika kumzidi Messi, kwa maana ya kwamba anacheza vizuri kwa miguu yote miwili, na anatumia vyema kichwa,’’ anasema staa wa zamani wa Valencia, Angel Dealbelt.

“Anaweza kupeleka mashambulizi mbele na kufumua mashuti, Messi kuna kitu anashindwa linapokuja kwenye kupiga mipira ya kichwa na kutumia mguu wa kulia,’’ anafafanua Dealbelt.

Carlo Ancelotti naye hahitaji kushawishiwa na yeyote kuhusu hilo, “Cristiano ni wa dunia nyingine, anafunga kwa staili inayofurahisha, ni vigumu kupata maneno sahihi ya kumuelezea.”

Na kama hiyo haitoshi, Ancelloti ambaye wakati kitabu hiki kikiandikwa alikuwa akiinoa Bayern Munich na sasa ni kocha wa Napoli anaongeza kuhusu Ronaldo.

“Bila ya kumdharau yeyote kwangu Cristiano Ronaldo ni mwanasoka bora kati ya wanasoka niliowahi kuwafundisha.”

Hata mwanariadha maarufu duniani, Usain Bolt naye ni shabiki wa staa huyu mwenye asili ya Ureno ambako anasema, “Ronaldo ni zaidi ya Messi, hakuna shaka katika hilo, ni mchezaji ambaye ana kila kitu,’’ anasema na kuongeza, “Zaidi ya hilo ni mchezaji na mtu mzuri.”

Vilevile tuna wajibu wa kumsikia Sir Alex Ferguson, “Watu wanasema nani mchezaji bora duniani kati ya Ronaldo na Messi huwezi kupingana na mawazo ya watu lakini Ronaldo anaweza kuchezea Millwall, Queens Park Rangers na Doncaster na akafunga hat-trick sina hakika kama Messi naye anaweza kufanya hivyo.’’

“Ronaldo ana miguu miwili ya soka, mwepesi na makini anapotumia mipira ya juu, kwangu nafikiri Messi ni mchezaji wa Barcelona.”

Kwa anachokisema Ferguson pengine ni muhimu kuzingatia mahali Ronaldo alipo kwa sasa, anaichezea Juventus ya Italia huku akiwa kinara wa mabao, maana yake kasi yake ya kuzifumania nyavu ni hiyo hiyo tangu akiwa Man United, Real Madrid na sasa Juventus.

Je, vipi kwa Messi angeyaweza hayo? Angeweza kufanya makubwa na klabu nyingine kama anavyofanya Ronaldo au anabaki kuwa ni mchezaji wa Barcelona kama anavyosema Ferguson? Bila shaka ni vigumu kuwa na jibu kwa sababu maisha ya Messi yameendela kuwa ya Barcelona.

Tangu mpambano wa wachezaji hao uwe wa ana kwa ana, wamekuwa wakichukuliwa na mashabiki wao kuwa ni wapinzani, na vyombo vya habari pamoja na mashabiki nao wameweka mkazo wao katika hilo tangu Ronaldo ajiunge na Real Madrid.

Wanapewa picha ya mastaa mahasimu wakubwa, kila mmoja akiwa mwenye uwezo wa kuufunika ubora au ukubwa wa mwenzake, mashabiki na watu wa Ronaldo wakati wote wamekuwa wakikataa kwamba Messi ni zaidi na ni hivyo hivyo kwa mashabiki wa Messi kwa Ronaldo.

Inapotokea mashabiki wao kokote duniani wanapoonyesha hasira zao humlinganisha mmoja dhidi ya mwenzake, na hata kwenye vyombo vya habari, swali ambalo wamekuwa wakiulizwa sana ni lile la kutaka maoni ya mmoja dhidi ya mwenzake, Ronaldo ataulizwa maoni yake kuhusu Messi na Messi naye ataulizwa kuhusu Ronaldo.

Itaendelea Jumanne ijayo…