MADENI: Wanadaiwa na timu zao

Muktasari:

Kikosi cha Taifa Stars kimesheheni wachezaji wengi wa Simba, Yanga na Azam FC ndio maana ili kuweka usawa na kuondoa migogoro na maneno ya hapa na pale, imebidi mechi zao zisimame kupisha ratiba ya mechi za kimataifa.

WABABE wa soka nchini Simba, Yanga na Azam FC mechi zao za Ligi Kuu zimesimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa 'Taifa Stars' kujiandaa na mchezo wao wa kuwania kufuzu fainali za Afcon 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon.
Stars itacheza dhidi ya Lesotho Novemba 16, katika mchezo ambao Stars inahitaji matokeo mazuri, ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kuhakikisha wanapata nafasi ya kushiriki michuano hiyo mwakani.
Hii haimaanishi ligi imesimama bali kuna baadhi ya timu ambazo zenyewe hazijatoa wachezaji wengi kwenye kikosi cha Stars zenyewe zitaendelea na michezo yao kama kawaida.
Stars imesheheni wachezaji wengi wa timu hizo za Simba, Yanga na Azam ndio maana ili kuweka usawa na kuondoa migogoro na maneno ya hapa na pale, imebidi mechi zao zisimame kupisha ratiba ya mechi za kimataifa.
Yote tisa, kuna wachezaji ambao walisajiliwa na klabu hizo na nyingine lakini mpaka sasa hawana la maana walilolifanya.
Ni wazi mzunguko wa pili utaanza baada ya dirisha dogo na kama hawajui tu, ni lazima wajitathimini na kuongeza juhudi ili kuwashawishi makocha na kuwaonyesha viongozi wao ni kwa nini waliamua kuwasajili wao na si wengine.

JOHN BOCCO -SIMBA
Alikuwa na msimu mzuri msimu wa kwanza alipojiunga na Simba na kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa ikiwa na pointi nyingi sambamba na uwingi wa mabao yaliyofungwa na nyota wa timu hiyo.
Bocco msimu ulioisha alifunga mabao 14 huku kinara wa upachikaji mabao Emmanueli Okwi akiwa na mabao 20 lakini hadi sasa pamoja na kupata nafasi ya kucheza amefunga mabao mawili tu hadi sasa ambayo yote aliyafunga mchezo dhidi ya Mwadui.

AMISS  TAMBWE- YANGA
Hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu baada ya kukumbwa na majeruhi yaliyomfanya kukaa nje ya dimba na kuonekana kama amesahaulika katika kikosi cha Yanga, kutokuwepo kwa mshambuliaji Herieter Makambo kulimshawishi kocha Mwinyi Zahera kumpa nafasi Tambwe dhidi ya Singida United.
Tambwe hakutaka mbwembwe zaidi ya kumdhihirishia kocha wake kuwa hakukosea kumpanga, na hapo aliiwezesha timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 2-0 yote yakifungwa na Mrundi huyo.
Mara ya mwisho Tambwe kufunga kwenye Ligi Kuu ilikuwa Mei 16 msimu wa 2016/17 walipocheza na Toto Africans hapa jiji Dar es Salaam hiyo ni kala ya mabao ya msimu huu.

DONALD NGOMA- AZAM FC
Ngoma aliyesajili  na Azam  akitokea Yanga alijiunga na matajiri hao wa jiji wakiwa na imani kuwa ataziba pengo la Bocco ambaye alikwenda Simba na hadi sasa bado nafasi hiyo imepwaya baada ya kumsajili Mbaraka Yusuph ambaye pia alishindwa kuziba pengo hilo.
Hadi sasa Ngoma amefunga mabao matatu katika michezo aliyocheza ni tofauti na alivyokuwa Yanga na uwezo wake ulivyo kwa ana jicho la kuona goli na amekuwa na muda mchache wa kucheza baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeruhi.

CLATOUS CHAMA - SIMBA
Hakuanza msimu na timu hiyo baada ya kibali chake kuchelewa, lakini muda mfupi aliokaa na timu hiyo ameonekana kufanya vyema hasa ile michezo ya kirafiki kabla ya msimu kuanza
Mzambia huyo alichukuliwa kutoka timu ya Lusaka Dynamos hadi sasa amefanikiwa kupachika mabao mawili na kufanikiwa kuibuka kuwa nyota anayezungumzwa sana midomoni mwa mashabiki wake ni kutokana na uchezaji wake pamoja na kufanya hivyo bado anadeni kubwa kwa mashabiki wa Simba.

ALEX KITENGE - STAND UNITED
Aliingia midomoni mwa watu baada ya kuifunga Yanga mabao matatu 'hat- trick' lakini tangu ameisaidia timu yake kuambulia idadi kubwa ya mabao bila pointi hajaweza kufanya jambo lingine hadi sasa.
Kitenge ni mshambuliaji wa kimataifa ameongezwa katika kikosi hicho kwa lengo la kuhakikisha anaisaidia timu kupachika mabao mengi zaidi na kuitengenezea nafasi nzuri katika msimamo wa ligi ni mapema sana kujaji uwezo wake kutokana na timu nyingi kucheza michezo michache.

HERITIER MAKAMBO- YANGA
Amesajiliwa akiwa kama mshambuliaji wa kuisaidia Yanga kuhakikisha inafunga mabao mengi zaidi tangu amejiunga na Yanga hadi sasa amepachika mabao manne tu kambani na ni chaguo la kwanza la kocha Mwinyi Zahera.
Matarajio ya uongozi mara baada ya kupata saini ya Mkongo huyo yamegeuka shubiri  kwani na sasa kuhaha kumtafuta straika mwingine wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Makambo ameshindwa kuendana na kasi ya timu kutokana na kukosa umakini na kushindwa kutumia nafasi nyingi anazotengenezewa.

ADAM SALAMBA- SIMBA
Ni miongoni mwa nyota waliosajiliwa Simba wakitokea klabu ndogo na ni nyota ambaye amepata nafasi ya kucheza japo kwa dakika chache tofauti na wengine ambao hawajapata kabisa nafasi hiyo.
Salamba hadi sasa amefunga mabao mawili tu katika mechi alizopata nafasi ya kucheza tofauti na Mohamed Rashid na nyota wengine wengi ambao walisajiliwa msimu huu wakiwa na kasi nzuri ya kufumania nyavu na sasa hawana nafasi kabisa ya kucheza.