Lyon, Coastal zatuziana heshima Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

Lyon inayofundishwa na Mreno Sococta Lwhel na Coastal inayonolewa na Juma Mgunda zimekuwa zikicheza soka la kushambuliana tangu mechi ilipoanza hadi mwisho.

Dar es Salaam. African Lyon imeshindwa kutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa suluhu Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Licha ya timu zote kucheza soka la kushambuliana kwa dakika 90 zilikosa umakini na ubunifu kwenye safu zao za ushambuliaji jambo lililofanya zipoteze nafasi nyingi za mabao.

Dalili za mechi hiyo kumalizika kwa sare zilianza kuonekana tangu mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kila upande licha ya kutengeneza nafasi nzuri za mabao, hazikuweza kutumika vyema na zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Coastal Union watazijutia dakika za mwanzoni mwa kipindi cha pili ambapo walipata nafasi nzuri zaidi ya Lyon ikiwemo ile ya Abushehe Issah dakika ya 53 aliyepoteza akiwa analitazama lango la Lyon baada ya shuti lake kugonga mwamba na kurudi uwanjani.

Kasi hiyo ya Coastal mwanzoni mwa kipindi cha pili iliilazimisha Lyon kufanya mabadiliko kwa kumtoa Gervas Bernard na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Omary ambayo yaliirudisha Lyon mchezoni na kuanza kujibu mashambulizi.

Mbali na mabadiliko hayo, Lyon pia iliwatoa Victor Da Costa na Awadh Juma huku nafasi zao zikichukuliwa na Salum Mdowe na Mtikila Said.

Coastal Union waliwatoa Moses Kitandu, Muhsin Malima huku nafasi zao zikichukuliwa na Mtenje Albano na Ayoub Lyanga.

Mabadiliko hayo hata hivyo hayakuweza kubadili taswira ya mchezo huo na kuzifanya timu hizo zigawane pointi.

Matokeo hayo yameifanya Coastal ifikishe pointi sita baada ya kucheza michezo minne huku Lyon ikifikisha pointi tatu.