Lwandamina apata mrithi wa Ngoma

Muktasari:

Yanga kwa sasa inajiandaa na mashindano ya kimataifa pamoja na kupigania kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam. YANGA imewapa mapumziko ya siku mbili nyota wake hadi kesho Jumapili kabla ya kuanza tizi kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui, lakini habari njema kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo ni kupatikana kwa mrithi wa Donald Ngoma.

Ngoma na Amissi Tambwe wamekosekana kwa muda mrefu ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na majeruhi na kuwapa presha Wana Jangwani, lakini Kocha kocha  George Lwandamina ametumia dakika 90 kugundua kitu kwa straika mpya chipukizi Yohana Mkomola na kutamka; "huyu akitulia anakinisikiliza atakuwa Ngoma mpya."

Mkomola aliyesajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo akitokea kikosi cha timu ya taifa ya vijana U17, amemkuna mno Mzambia Lwandamina na kudai kama akituliza akili akawasikiliza makocha wake atakuwa ni mwiba mkali ndani ya uwanja.

Lwandamina alisema aliyeamua kukaa jukwaani katika mchezo wa mwisho kati ya Yanga dhidi ya URA na timu yake kung'olewa michuano ya Mapinduzi kwa matuta,  aligundua kwamba Mkomola ni moja ya kipaji bora walichonacho katika safu yao ya ushambuliaji.

Lwandamina alisema Mkomola ni moja katia ya usajili bora waliowahi kuufanya ambapo kama ataendelea kuwa msikivu na kudumisha nidhamu atakuwa na msaada mkubwa katika kikosi hicho katika michezo ya Ligi Kuu na hata kimataifa.

Alisema kinda huyo anaonekana kuwa na makali mengi ikiwemo kasi akiwa pia na ubora wa kujua kujitenga katika maeneo mazuri ya kufunga ambapo bado vitu vichache vinapungua ambavyo atamuongezea taratibu.

"Angalia akitoa pasi anachofanya hazubai anakimbilia sehemu sahihi kusubiri afunge pia anapenda kuhakikisha kama hapa kipa kashadaka au nafasi imepotea ni moja kati ya vipaji bora tumevipata," alisema Lwandamina.

"Ukiwa kocha sio kila wakati utapata mchezaji aliyekamilika kuna vitu vimepungua kwake nitapambana kumbadilisha taratibu, lakini naamini kama akiwa msikivu na akidumisha nidhamu nitamfanya kuwa mchezaji bora katika safu ya ushambuliaji.

"Uwezo wake ni kama alionao Ngoma ambaye kwa muda mrefu amekuwa nje ya uwanja, ila Mkomola akikaa sawa atafukia mashimo yote ya safu ya ushambuliaji."