Lusajo ataka kumpindua Kagere

Muktasari:

Kitendo cha straika wa Simba, Meddie Kagere kuchukua kiatu cha dhahabu mara mbili mfululizo ni kama kimemuamsha mshambuliaji wa KMC, Reliants Lusajo kutaka kupindua meza msimu huu.

STRAIKA wa KMC, Reliants Lusajo amesema licha ya Ligi Kuu Bara, kuonekana ina ushindani wa hali ya juu msimu huu, anaamini hilo sio sababu ya kumzuia kuingia kwenye kinyang'anyiro cha Mfungaji Bora.

Msimu ulioisha Lusajo akiwa na Namungo FC alimaliza na mabao 13, jambo ambalo anataka kuanza na kuvunja rekodi hiyo, kisha kuandika nyingine itakayoendelea kumpa thamani ya kuwa straika mwenye kuacha alama kwenye ligi inayoendelea.

Amesema kwa mechi tatu ambazo zimechezwa mpaka sasa, ameona jinsi ambavyo wachezaji wana mwamko wakufanya kitu kuzisaidia timu zao, kitu anachoona kitazalisha ushindani na viwango vya juu kwao kama wachezaji.

Jana Jumatatu, Lusajo alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi tangu msimu uanze dhidi ya Mwadui FC ambapo KMC walishinda bao 2-1, mabao yote ya KMC yalifungwa na Lusajo.

"Kwanza nataka nianzie pale nilipoishia msimu ulioisha, baada  ya hapo naingia  kwenye kinyang'anyiro cha kuchukua kiatu cha dhahabu ambacho kinamilikiwa na  Meddie Kagere wa Simba mara mbili mfululizo,"amesema Lusajo na ameongeza kuwa.

"Pamoja na ligi kuwa ngumu inasaidia wachezaji kujituma na ndani ya kujituma kunakuwa na kiwango cha juu ambacho kitakuwa kinawapa burudani mashabiki wanaofika uwanjani kutazama mechi,"amesema.

Lusajo amesema kama kuna kitu kinamuumiza ni kuona kiatu hicho kinatawaliwa na mastaa wa kigeni kwa muda mrefu, jambo analoona linawaamsha na kuwapa ari ya kujituma ili kuondoa hilo.

Kabla ya Kagere ambaye mara ya kwanza alifunga mabao 23 na msimu uliopita alifikisha mabao 22, Emmanuel Okwi raia wa Uganda wakati huo anaichezea Simba aliibuka mfungaji bora akiwa amefunga mabao 19.

 

"Lazima tupambane kwa kadri tunavyoweza kwani kitendo cha wageni kuchukua kiatu kila wakati,  kinakuwa kinatuletea picha mbaya, ila msimu huu lazima tujipange upya ili tupindue meza,"amesema.