VIDEO> Lunyamila: Simba haitakiwi kufanya makosa

Muktasari:

Amesema kuwa tayari timu hizo zinafahamiana vizuri na kuwa kila atakayefanya makosa ataadhibiwa.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Edibily Lunyamila amewataka wachezaji wa Simba kujituma katika mchezo wa leo Jumamosi Machi 16, 2019 dhidi ya AS Vita kwa kuwa hata wenyewe wanataka nafasi.

Lunyamila amesema kuwa Wacongoman hao waliingia fainali msimu uliopita kwenye Kombe la Shirikisho, wakapoteza fainali, lakini leo watataka kuonyesha hawakubahatisha na kwamba na wenyewe wanaitaka nafasi.

Amesema kuwa tayari timu hizo zinafahamiana vizuri na kuwa kila atakayefanya makosa ataadhibiwa.

Lunyamila ambaye kwa sasa ni kocha wa Shule ya Sekondari ya Kenton, Tabata amesema kwa kuwa Simba wameuona mchezo wa kwanza na wameshafahamu ukali na udhaifu wa wapinzani wao, wanatakiwa wasifanye makosa mengine.

"Ngome tuliona ilifanya makosa mengi mchezo wa kwanza, kipa alikuwa akishindwa kujipanga, lakini ninaamini kocha ameyafanyia kazi makosa hayo na nina imani Simba itapata matokeo.

"Ninaamini kwa kuwa Simba wako nyumbani, na wameshajifunza na makosa yaliyopita, watapata matokeo lakini kinachotakiwa ni Simba kufunga bao la mapema ambalo kwanza litawapa hamasa Simba pamoja na mashabiki wake kuwa na nguvu ya kushangilia lakini pia litawachanganya AS Vita."