Lulu amaliza kifungo

Muktasari:

April 26, 2018, Lulu alikuwa mmoja wa wafungwa walionufaika na msamaha wa Rais John Magufuli wakati wa kuadhimisha miaka 54 ya Muungano. Alisamehewa robo ya adhabu yake hivyo kifungo chake kitaishia Novemba 12, 2018.

Jana Jumatatu  msanii mwigizaji wa filamu maarufu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ alianza ukurasa mpya wa maisha huru baada kumaliza kutumikia adhabu yake aliyohukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Lulu alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela Novemba 13, 2017 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia, mpenzi wake ambaye pia alikuwa mwigizaji wa filamu maarufu ndani na nje ya nchi, Steven Kanumba, Aprili 7, 2012.

Makala haya ya Maisha ya Lulu katika kesi ya kifo cha Kanumba ni kumbukumbu ya mtiririko wa matukio muhimu aliyoyapitia msanii huyo kwa muhtasari katikati ya kesi tangu kukamatwa na kushtakiwa hadi kumaliza adhabu.

Aprili 6/7, 2012: Ugomvi/kifo cha Kanumba

Saa sita kasoro dakika kadhaa usiku Lulu alifika nyumbani kwa Kanumba maeneo ya Sinza Vatican baada ya kuitwa na Kanumba, ili amuage kwa kuwa alikuwa anakwenda disko na rafiki zake. Mara unaibuka ugomvi baina yao na hatimaye Kanumba anaanguka na kufariki dunia.

Aprili 7, saa 11 alfajiri Lulu alitiwa mbaroni na askari polisi kutoka kituo cha Polisi Oysterbay, Ester Zefania, eneo la Bamaga kwa msaada wa mtego kupitia mawasiliano yake na daktari binafsi wa Kanumba, Dk Paplas Kagaiya.

Aprili 8, askari Ester alimpeleka Lulu katika hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu baada ya kulalamika kuwa anasikia maumivu (kutokana na kipigo alichodai kupewa na mpenzi wake (Kanumba).

Apandishwa kizimbani, gerezani

Aprili 10, Lulu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando na kusomewa shtaka la kuua, kumuua Steven Kanumba kwa kukusudia.

Shtaka hilo halina dhamana, hivyo alianza maisha mapya katika mahabusu ya gereza la Segerea, wakati kesi yake ikiendelea.

Aprili 23, mawakili wanne walijitokeza kumtetea Lulu akiwamo aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Joaquine De- Melo, ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na pia mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King. Joaquine sasa ni jaji.

Wengine ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

Utata wa umri waibuka

Mei 7, mawakili wa mshtakiwa huyo waliwasilisha maombi ili msanii huyo ashtakiwe katika Mahakama ya Watoto, wakidai ana umri wa miaka 17.

Hakimu Mmbando aliyakataa na kuwataka mawakili wa msanii huyo kuwasilisha maombi yao Mahakama Kuu.

Mei 15, mawakili wa msanii huyo waliwasilisha maombi Mahakama Kuu, wakiiomba iamue kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kufanya uchunguzi wa umri wake halisi au Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Mei 28, maombi hayo yanasikilizwa na Jaji Dk Fauz Twaib. Upande wa mashtaka unaweka pingamizi kuwa vifungu vya sheria vilivyotumika kufungua maombi haviipi mahakama hiyo mamlaka ya kuyasikiliza.

Juni 11, Mahakama Kuu ilitupilia mbali pingamizi la upande wa mashtaka kuwa haina uwezo wa kufanya uchunguzi huo, badala yake iliamua kuwa inao uwezo wa kufanya na ikapanga kuuanza Juni 25.

Juni 25, Mahakama yasitisha uchunguzi, Lulu amwaga machozi. Mahakama Kuu ilisitisha kuendelea na uchunguzi wa umri wa mshtakiwa, baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa uliwasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya mapitio ya uamuzi wa Jaji Twaib. Uamuzi huo ulimfanya Lulu kumwaga machozi kizimbani kimyakimya.

Oktoba 5, Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani chini ya majaji Januari Msoffe, Bernard Luanda na Edward Rutakangwa lilitoa uamuzi kuhusu utata wa umri ambapo iliirudisha kesi hiyo Kisutu iendele na taratibu za kawaida.

Desemba 17, Upande wa mashtaka uliieleza Mahakama ya Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na unambadilishia shtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa la kuua bila kukusudia, taarifa ambazo zilimfanya mshtakiwa huyo kuonyesha furaha yake.

Desemba 21, Lulu alisomewa shtaka jipya la kuua bila kukusudia baada ya kubadilishiwa kutoka shtaka la kuua kwa kukusudia.

Kisha alisomewa maelezo ya mashahidi wa upande wa mashtaka na vielelezo vitakavyotolewa mahakamani wakati wa usikilizwaji kama sehemu ya ushahidi.

Hakimu Mmbando alitangaza kufunga rasmi jalada la kesi hiyo mahakamani hapo na kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kamili.

Januari 22, 2013, kupitia kwa jopo la mawakili wake, Lulu aliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu baada ya kubadilishiwa shtaka kutoka la kuua na kuwa la kuua bila kukusudia kwa kuwa hilo linadhaminika.

Januari 28, Maombi ya dhamana ya msanii huyo yalisikilizwa na Jaji Zainabu Muruke na kumpa dhamana kwa masharti maalumu, baada ya upande wa mshtaka kusema hauna pingamizi.

Jaji alimtaka Lulu kusaini bondi ya Sh40 milioni, kuwasilisha hati ya kusafiria kwa msajili wa mahakama hiyo na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila idhini ya msajili wa mahakama.

Mengine ni kuripoti kwa msajili kila tarehe moja ya mwezi hadi kesi yake ya msingi itakapomalizika, kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini na kila mmoja kusaini bondi ya Sh20 milioni.

Alikamilisha masharti, lakini alikwama na kurudi mahabusu kutokana na msajili ambaye anatakiwa kuthibitisha kama amekidhi masharti kutokuwepo.

Januari 29, Lulu alitoka mahabusu na kurejea uraiani baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.

Februari 18, 2014: Kwa mara ya kwanza Lulu aliruhusiwa kujibu shtaka. Alisomewa maelezo ya kesi mbele ya Jaji Rose Teemba, kisha alitakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo.

Alikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba, lakini alikana kuhusika na kifo chake.

Oktoba 19, 2017: Kesi ilianza rasmi kusikilizwa na upande wa mashtaka ulianza kutoa ushahidi wake na kuwasilisha mahakamani vielelezo mbalimbali vya ushahidi.

Oktoba 23, upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya shahidi wa nne kumaliza kutoa ushahidi. Mahakama ilitoa uamuzi kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu na kumtaka ajitetete.

Lulu alijitetea akiongozwa na Wakili wake Peter Kibatala. Katika utetezi wake alikana kuhusika na kifo hicho.

Oktoba 26, Wakitoa maoni yao, Washauri wa Mahakama wote watatu walimtia hatiani kuhusika na kifo cha mpenzi wake bila kukusudia.

Novemba 13, saa 5.04-5.05 asubuhi, Jaji Rumanyika alimhukumu kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumuua mpenzi wake, Steven Kanumba bila kukusudia. Alipokewa gerezani na kupewa namba ya usajili, Mfungwa Na. 1086/2017. Alisamehewa theluthi moja ya adhabu yake (miezi minane), hivyo kifungo chake kitaishia Machi 12, 2019, badala ya Novemba 12, 2019.

Msamaha wa Rais

April 26, 2018, Lulu alikuwa mmoja wa wafungwa walionufaika na msamaha wa Rais John Magufuli wakati wa kuadhimisha miaka 54 ya Muungano. Alisamehewa robo ya adhabu yake hivyo kifungo chake kitaishia Novemba 12, 2018.

Mei 12, Lulu aliachiwa huru kutoka gerezani baada ya kubadilishiwa adhabu kwenda kutumikia kifungo cha nje cha adhabu yake iliyokuwa imebakia, kwa amri ya Mahakama Kuu. Alipangiwa kufanya usafi ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Novemba 13, Hatimaye Lulu anakuwa raia huru baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kufanya shughuli za kijamii. Ukurasa wa maisha yake ndani ya kesi umefungwa rasmi, anarejea katika maisha ya awali.