Lugha kwao sio tatizo

Thursday March 14 2019

 

LONDON, ENGLAND.KWENDA shule pamoja na kucheza katika nchi mbalimbali kunawafanya mastaa wengi wa soka wajifunze na kujua kuongea lugha za nchi nyingi mbalimbali.

Hata hivyo, kuna wanasoka ambao wamepitiliza kwa kujua kuzungumza lugha nyingi mbambali.Wafuatao wanazugumza lugha nyingi zaidi.

Romelu Lukaku (lugha 8)

Staa wa kimataifa wa Ubelgjji ambaye kwa sasa anatisha katika safu ya ushambuliaji ya Manchester United. Akiwa amezaliwa jijini Antwerp nchini Ubelgiji na wazazi wa Kicongo, Lukaku alijifunza nyumbani lugha za Kifaransa, Kilingala na Kiswahili cha Congo.

Kutokana na kukulia Ubelgiji nchi ambayo pia inatumia lugha ya Kidachi, Lukaku pia anazungumza Kidachi. Akiwa Shule, Lukaku pia alijifunza Kiingereza na Kihispaniola.

Wakati akiichezea Anderlecht mechi ya kwanza Lukaku alikuwa na umri wa miaka 16 na tayari alikuwa anaweza kuzungumza lugha sita. Akiwa na Anderlecht alikutana na wanasoka wengi wa Brazil na akajikuta anaongea lugha ya Kireno. Lukaku pia anaelewa Kijerumani.

Henrikh Mkhitaryan (lugha 7)

Orodha hii ya wachezaji wanaozungumza lugha nyingi haiwezi kukamilika kama hautamtaja staa huyu wa ikimataifa wa Armenia ambaye alijiunga na Arsenal katika dirisha dogo la uhamisho la mwaka jana akitokea Manchester United.

Staa huyu wa zamani wa Borussia Dortmund ana uwezo wa kuongea lugha saba za ufasaha. Anaweza kuongea lugha ya kwao Armenia, anaweza kuongea Kiingereza, pia anaweza kuongea Kijerumani ambako alijifunza wakati anacheza Dortmund huku pia akifahamu lugha ya Kirusi baada ya kucheza Shakhtar. Kiungo huyu mwenye uwezo mkubwa wa kutumia miguu yake miwili kwa pamoja ana uwezo pia wa kuongea lugha za Kiitaliano, Kifaransa na Kireno.

Petr Cech (Lugha 5)

Kipa wa kimataifa wa Czech ana maajabu yake. Anaweza kuupanga ukuta wake kwa lugha tofauti kutegemea na uraia wa mabeki wake. Anazungumza lugha tano kwa ufasaha na anatumia lugha hizo kuwapanga mabeki wake. Achilia mbali lugha ya kwao Czech, Cech ana uwezo wa kuongea Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kihispaniola.

Aliwahi kukaririwa akielezea jinsi anavyoweza kuupanga ukuta wake kutegemeana na lugha za mabeki wake. “Naongea na mabeki wangu wa pembeni (Hector Bellerin, Nacho Monreal) kwa Kihispaniola, naongea na (Laurent) Koscielny kwa Kifaransa na naongea na Per (Mertesacker) kwa Kiingereza.”

Aliwahi kukaririwa akisema hivyo mwaka 2015. “Wakati mwingine mchezaji wa kigeni anaweza asielewe unachosema. Unapojua hilo inakuwa rahisi wakati mwingine kuongea kwa lugha yao ukitazamia kwamba wataelewa.”

Jose Mourinho(Lugha 6)

Kocha mbwatukaji ambaye amekuwa akileta utata mkubwa katika vyombo vya habari. Achilia mbali lugha yao ya kwao ya Kireno lakini Mourinho amekuwa hapati shida kuwasiliana na wachezaji wake akitumia lugha mbalimbali.

Mourinho ana uwezo wa kuongea pia Kihispaniola, Kiitaliano, Kifaransa na Kiingereza ambacho alikitumia siku ya kwanza tu alipotambulishwa kuwa kocha mpya wa Chelsea mwaka 2004 huku akijiita Special One.

Mourinho pia anazungumza lugha ya Catalunya ambayo aliijua wakati akiwa kocha msaidizi pale Barcelona. Uwezo wake wa kuzungumza lugha nyingi tofauti ulisababisha aitwe jina la ‘Mkaliman’ ingawa mwenyewe hakulipenda jina hilo.

Zlatan Ibrahimovic (Lugha 6)

Mmoja kati ya mastaa wa soka waliozurura zaidi katika klabu mbalimbali za Ulaya. Nyota huyu amewahi kuzurura katika klabu za FC Barcelona, Paris Saint-Germain, Manchester United, Juventus, Inter Milan, Ac Milan na Ajax.

Ibrahimovic ana uwezo wa kuongea lugha sita tofauti akianzia lugha ya kwao Sweden ambako amezaliwa na kukulia. Pia anafahamu Kibosnia ambayo ni ya wazazi wake waliohamia Sweden wakitoka Ulaya Mashariki katika nchi ya Bosnia.

Achilia mbali lugha hizo pia Zlatan ana uwezo wa kuzungumza Kiingereza kama alivyokuwa akisikika wakati akicheza Manchester United pale England. Ana uwezo wa kuzungumza Kiitaliano baada ya kucheza soka Italia kwa muda mrefu, pia anaweza kuzungumza Kihispaniola na Kifaransa.

Hili halishangazi sana hasa kwa mchezaji kama yeye ambaye amekuwa mzururaji kwa muda mrefu katika soka.

Advertisement