Luc ageuka bubu kwa Morrison

Muktasari:

Morrison amekuwa akihusishwa kujiunga na Simba hivyo matukio anayoyafanya baadhi ya mashabiki wana amini kwamba mchezaji huyo amesaini kweli kwa wapinzani wao.

Tukio la winga wa Yanga, Benard Morrison kuonyesha utovu wa nidhamu dakika ya 65 alipotolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Patrick Sibomana limeibua mijadala mbalimbali mitandaoni.

Winga huyo alipotolewa alionyesha kuchukia na kutoka moja kwa moja kwenda vyumbani, lakini wakati akiwa anatoka muamuzi wa mezani Nadeem Aloyce alimzuia lakini mchezaji huyo alionyesha kutokubali kabisa kurejea kukaa katika benchi.

Morrison alipoingia vyumbani, hakutaka kabisa kukaa humo humo na kusubili mchezo umalizike badala yake alitoka na kuongozana na ndugu zake na kupotea kabisa uwanjani.

Mwanaspoti lilimtafuta kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael aweze kuzungumzia tukio hilo yeye akiwa kama ndio muongoza jahazi lakini alipata kigugumizi.

Eyamael alisema "Siwezi kuzungumza lolote".

Hii inakuwa ni tukio la pili kwa Morrison kuwa juu ya Yanga baada ya awali kuwaanika viongozi wa Yanga hadharani kwamba hana mkataba na timu hiyo kiasi cha kupelekana katika kamati ya sheria na hadhi za wachezaji.