Los Angeles, Miami kuuana fainali Alhamisi

Dar es Salaam. Nyota wa ligi ya kikapu Marekani (NBA), LeBron James ataiongoza Los Angeles Lakers kucheza fainali ya kwanza baada ya miaka 10, dhidi ya timu yake ya zamani, Miami Heat.

LeBron aliwahi kuichezea Miami Heat na kuipa mataji mawili ya NBA timu hiyo 2012 na 2013, yakiwa ni mataji yake ya kwanza kutwaa, huku taji lake la tatu akilitwaa akiwa na Clevaland Cavaliers 2016.

Baada ya kushindwa kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza msimu uliopita, ambao ndio ulikuwa wa kwanza kwake kuichezea Los Angeles Lakers, LeBron amefanikiwa kuiongoza timu hiyo kufuzu fainali baada ya ushindi wa jumla wa 4-1 dhidi ya timu iliyokuwa bora msimu huu, Denver Nuggets.

Matokeo hayo yaliwapa rekodi tamu Lakers kwenye hatua ya mtoano hadi fainali ya ukanda wa Magharibi, awali waliifunga Portland Trail Blazer 4-1 na Houston Rockets kwenye nusu fainali waliwachapa 4-1.

Kazi nzuri ya LeBron James aliyefunga ‘triple-double’ mbili kwenye fainali na kumfanya afikishe jumla ya triple-double 27 za hatua hiyo, huku pia akiongeza rekodi yake ya kucheza jumla ya fainali 10 katika misimu 17 aliyocheza NBA.

Miami Heat wakiongozwa na Jimmy Butler, walifanikiwa kutinga fainali kwa kuibuka mabingwa ukanda wa Mashariki, wakiiondosha mabingwa mara nyingi kihistoria wa ligi hii, Boston Celtics waliotwaa mataji 17, kazi nzuri ya Bam Adebayo kwenye mchezo wa sita jana, uliwapa ushindi wa jumla Miami Heat 4-2 Boston Celtics.