Ljungberg kumweka kitako Pepe, Arsenal ikivaa Brighton leo

Muktasari:

Hakuanzishwa kwenye mechi nne kabla ya usiku wa jana Alhamisi na aliishia kuketi kwenye benchi tu katika mechi ya 2-2 dhidi ya Norwich City, ambayo ilikuwa ya kwanza chini ya kocha mpya Ljungberg.

LONDON, ENGLAND.KOCHA wa mpito kwenye kikosi cha Arsenal, Freddie Ljungberg amesema atafanya mazungumzo ya kina na mchezaji ghali wa timu hiyo Nicolas Pepe baada ya kuonekana kuteseka na maisha ya Ligi Kuu England.

Arsenal ilizama mfukoni na kutumia Pauni 72 milioni kunasa saini ya mshambuliaji huyo kutoka Lille kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini staa huyo wa kimataifa wa Ivory Coast kiwango chake kimekuwa cha kupanda na kushuka tangu alipotua Emirates.

Hakuanzishwa kwenye mechi nne kabla ya usiku wa jana Alhamisi na aliishia kuketi kwenye benchi tu katika mechi ya 2-2 dhidi ya Norwich City, ambayo ilikuwa ya kwanza chini ya kocha mpya Ljungberg.

Kocha huyo raia wa Sweden amechukua mikoba ya kuinoa Arsenal baada ya timu hiyo kumfuta kazi Unai Emery wiki iliyopita na anaamini kwamba Pepe wakati wake mzuri utakuja tu katika kikosi hicho.

“Nicolas ni mchezaji mzuri sana,” alisema Ljungberg na kuongeza. “Wakati mwingine tunatoka kwenye ligi tofauti hivyo inahitaji muda mrefu kuzoea mazingira ndani na nje ya uwanja. Nicolas ni moja ya watu hao na nimepanga kufanya naye mazungumzo ya kina yatakayomfanya awe vizuri. Yeye ni mchezaji muhimu sana kwetu. Nitamwambia kile ninachokitarajia na ninavyotaka acheze.”

Arsenal usiku wa jana Alhamisi walikuwa na kibarua cha kuwakabili Brighton kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uwanjani Emirates.