Liverpool yapata pigo

Muktasari:

Fabinho alianza kucheza kama beki wa kati baada ya Virgil van Dijk kupata majeraha ambayo yatamuweka nje kwa msimu mzima.

LIVERPOOL, ENGLAND. MCHAKA mchaka wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya iliendelea jana Jumanne ambapo Liverpool ilishinda mabao 2-0 dhidi ya FC Midtjylland. Mabao hayo yalifungwa na Diogo Jota na Mohamed Salah.

Katika mchezo huo Liverpool ilipata pigo lingine baada ya Fabinho ambaye alikuwa anaziba pengo la beki kisiki aliyeumia Virgil van Djik naye kupata majeraha yaliyosababishwa atolewe nje dakika ya 30 katika kipindi cha kwanza.

Baada ya kutolewa nje nafasi yake ilichukuliwa na kinda wa kikosi cha vijana Rhys Williams ambaye aliionesha kiwango kikubwa kilichowakosha mashabiki wengi akitumia zaidi ya dakika  70 kuiongoza safu ya ulinzi isiruhusu bao lolote na akafanikiwa.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema mchezaji huyo ameonesha kiwango kikubwa lakini benchi lake la ufundi litakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwa kuwa watu wengi wanamzungumzia jambo ambalo linaweza kushusha kiwango chake katika mchezo ujao wa Ligi Kuu na West Ham.

Mechi nyingine zilizopigwa jana ni kati ya Atalanta iliyokuwa nyumbani kuialika Ajax na mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 2-2. Huku mabingwa watetezi wa michuano hiyo Bayern Munich ikifanikiwa kushinda mabao 2-1 ugenini dhidi ya Lokomotiv Moscow.

Atletico Madrid ikiwa nyumbani ikaibamiza mabao 3-2 Salzburg ya Austria huku staa wao Joao Felix aliingia kambani mara mbili kuikoa Atletico ambayo ilitanguliwa kabla ya kusawazisha na kushinda.

Real Madrid ilionyesha kiwango kibovu baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Borussia Moenchengladbach huku Shakhtar Donetsk ikilazimishwa sare tasa na Inter  Milan.

FC Porto iliyokuwa nyumbani kwake huko Ureno ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Olympiacos. Manchester City ikashindi  mabao 3-0 dhidi ya Marseille.