Liverpool waambiwa ruksa kumzuia Salah

Muktasari:

Lakini, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameambiwa na Fifa kwamba anaruhusiwa kuzuia mshambuliaji wake Mo Salah kwenda Japan kitu ambacho kitamfanya akose mechi za maandalizi ya msimu ujao.

LIVERPOOL, ENGLAND . SHIRIKISHO la soka la kimataifa (Fifa) limethibitisha kwamba Liverpool wanaweza kumzuia supastaa wao Mohamed Salah asiende kwenye mashindano ya Olimpiki ya Tokyo.
Kocha wa timu ya soka ya taifa ya Misri kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23, Shawky Gharib amefichua kwamba mpango wake ni kumteua supastaa wa Liverpool kwenye orodha ya wachezaji watatu wenye umri mkubwa kuingia kwenye kikosi chake kwa ajili ya mashindano hayo yatakayofanyika mwishoni mwa Julai na wiki mbili za mwanzo za Agosti.
Lakini, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameambiwa na Fifa kwamba anaruhusiwa kuzuia mshambuliaji wake Mo Salah kwenda Japan kitu ambacho kitamfanya akose mechi za maandalizi ya msimu ujao.
Liverpool italazimika kuwaruhusu Salah, Sadio Mane na Naby Keita kwenda kucheza michuano ya Afcon Januari mwakani kama watachaguliwa kwenye vikosi vyao na jambo hilo litawafanya wakose huduma ya wachezaji wake kwa wiki zisizopungua sita.
Kwenye michuano hiyo ya Afcon, Liverpool haitakuwa na nguvu ya kuzuia wachezaji wake wasiende kama wakichaguliwa, lakini wanaruhusiwa kuzuia kwenye mashindano ya Olimpiki kwa sababu haipo kwenye kalenda ya mashindano ya Fifa.
Msemaji wa Fifa alisema: “Mashindano ya soka kwenye Olimpiki, pamoja na michuano mingine ya Fifa inayopangwa kwa kuzingatia umri haipo kwenye orodha ya mechi za kimataifa kwa timu za wanaume kwa mwaka 2018-2024, hivyo klabu hazitakuwa na ulazima wa kuruhusu wachezaji wake kwenda kucheza michuano hiyo."
Gharib anataka kumjumuisha Salah kwenye kikosi chake kwa sababu anaamini ni moja kati ya wanasoka watatu bora duniani.