Liverpool kumjaza mihela Van Dijk

Muktasari:

Ofisa Mkuu wa Uendeshaji kwenye klabu ya Liverpool, Andy Hughes alisema uwekezaji huo si wa kitoto hasa kwenye soka linalowahusisha klabu zinazotumia pesa kwa wingi kama Real Madrid , Barcelona na Manchester United .

LIVERPOOL, ENGLAND . LIVERPOOL wapo vizuri asikwambie tu. Ubora wao wa ndani ya uwanja umewafanya kupiga pesa za maana na kuwa moja ya klabu inayolipa vizuri mastaa wake duniani.
Nguvu hiyo ya kipesa ndiyo inayowafanya wawatulize mastaa wake kama Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino, ambao wote hao walipata dili za pesa nyingi mwaka jana na sasa wanataka kulifanya hilo kwa beki wao kisiki uwanjani, Virgil van Dijk.
Baada ya kupiga faida kubwa, Liverpool imechukua uamuzi wa kuwaongezea mishahara mikubwa mastaa wake muhimu kuendelea kubaki Merseyside kwa muda mrefu.
Taarifa ya klabu ilisomeka hivi kwamba mastaa kama Alisson, Keita, Fabinho na Shaqiri wamesaini mikataba mipya sambamba na wakali wengine, Jordan Henderson, Firmino, Salah, Mane, Robertson na Alexander-Arnold.
Ofisa Mkuu wa Uendeshaji kwenye klabu ya Liverpool, Andy Hughes alisema uwekezaji huo si wa kitoto hasa kwenye soka linalowahusisha klabu zinazotumia pesa kwa wingi kama Real Madrid , Barcelona na Manchester United .
Liverpool kwa sasa wanashika namba tatu kwenye Ligi Kuu England kwa timu zinazogawa mishahara mikubwa baada ya sasa wakipata kumpa dili jipya Van Dijk litakalomfanya awe beki anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani.
Kocha Jurgen Klopp naye amesainishwa mkataba mrefu wa kubaki Anfield huku dhamira ya kubwa ikiwa kuwabakiza kwenye kikosi mastaa wote wenye inayowaamini kwamba wana vipaji vya hali ya juu.