Liverpool hii inastahili kila kitu EPL, UCL

Saturday May 11 2019

 

KUNA wakati hutokea kwa timu kupata ushindi kwa sababu ya kuwa na bahati, lakini ushindi wa Liverpool dhidi ya Barcelona ulikuwa wa kustahili kutokana na jinsi mechi ya kwanza baina ya timu hizo ilivyochezwa.

Niliishuhudia mechi hiyo ya kwanza na nikawa na matumaini makubwa ya Liverpool kupata ushindi kwani waliutawala mchezo dhidi ya Barcelona ila kukosa nafasi tele za kufunga mabao.

Nikiwa mchezaji niliyechezea kufikia kiwango cha Ligi Kuu ya Kenya kati ya miaka 1977- hadi 1980 nikiwa na timu za Liverpool na Black Panther FC za Mombasa, nilihisi ushindi wa Barca ulikuwa haustahili, ilikuwa makosa ya madogo ya mabeki ndipo mabao yalipatikana.

Nilikuwa na maoni sawa na aliyekuwa Kocha wa Chelsea na Manchester United, Jose Mourinho, lakini hapo hapo kwa yale mapenzi ya timu yangu hiyo ya Liverpool, nilitofautiana naye kuwa tunaweza kupata ushindi mkubwa wa kutufanya tufuzu kwa fainali.

Kwa fikra zangu, niliamini kwa mchezo waliocheza huko Uhispania, nilikuwa sina wasiwasi ya kupata ushindi lakini nilijua tunaweza kupata ule wa bao 1-0, 2-0, 2-1, 3-1 ama 4-2 sikuweza kuwa na imani ya Liverpool kuweza kumaliza udhia kwa kuifunga Barcelona 4-0.

Nilitamani ningekuwa pamoja na shabiki mwenzangu wa Liverpool aliyeishuhudia mechi hiyo hapo Anfield, Hashim Ahmed Hadi, ambaye naye alikuwa uwanjani hapo pamoja na babake Divock Origi, Mike Okoth aliyewahi kuichezea timu ya taifa ya Kenya.

Advertisement

Hadi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa ofisa wa cheo cha juu wa timu niliyocheza ya Liverpool, alisema hajawahi kushuhudia dimba lililompendeza kama hilo hasa namna wachezaji walivyosakata soka la hali ya juu na kucheza kwa kujitolea mhanga hadi kupata ushindi.

Ni jambo la kufurahisha kuwa hivi sasa timu za Uingereza ndizo zilizofuzu kwenye fainali za vikombe vyote viwili vya Uropa. Liverpool itapambana na Tottenham katika fainali ya Champions League ambayo haitabiriki na matokeo yoyote yanaweza kupatikana.

Nazo timu mbili nyingine za hapo England, Arsenal na Chelsea zitagombania kombe la Uropa. Hii inadhihirisha wazi kuwa Ligi Kuu ya England ndiyo ngumu zaidi ya hizo nyinginezo.

Kuna wakati mwingine hata ukipenda, unastahili kufikiria mambo na kusema ukweli. Nilikuwa na hamu timu yangu ya Liverpool kushinda taji la Ligi Kuu ya England kuliko Kombe la Champions League lakini kwa jinsi ilivyo, sidhani kama hilo litawezekana.

Manchester City inapambana na Brighton siku ya Jumapili kwenye mechi ambayo City inahitaji kushinda ili iibuke washindi hali nayo Liverpool yangu itahitaji kushinda dhidi ya Wolves na wapinzani watoke sare ama washindwe ndipo kombe liwe Anfield.

Kwa uzuri wa timu, Man City wako bora kuliko Brighton hata kama watacheza mechi hiyo ugenini hali nayo Wolves ni ngumu zaidi ya Brighton, hivyo matumaini ni ya City kuhifadhi ubingwa wao.

Ni hadi maajabu yajitokeze ndipo nitafurahikia hamu yangu ya kushinda taji la Ligi Kuu. Kwa Champions League hainitii hamu sana kwani ningali natamba kuwa klabu ya England iliyochukua kombe hilo mara nyingi zaidi.

Sipendi wachezaji wetu wawe na ‘over confidence’ watakapocheza dhidi ya Tottenham kwani wapinzani wetu hao wanajulia mchezo wetu na pia watacheza kufa kupona kuhakikisha wanaweka historia ya klabu yao ya kushinda taji la Champions League.

Hata hivyo, siwezi kusema ninakwenda vitani kushindwa. Nina imani kubwa kwa hali ya mchezo tunaocheza wakati huu, hatustahili kumaliza msimu mikono mitupu.

Jurgen Klopp amekitengeza kikosi cha kutoa burudani siyo kwa mashabiki wa timu hiyo pekee bali kucheza soka linalowafurahisha wapenda soka wote ulimwenguni.

Nani anayepinga kutokana na tunavyosakata soka, tunastahili kushinda mataji yote mawili?

Advertisement