Liverpol yabeba ubingwa England

Liverpool, England. BAADA ya kusubiri kwa miaka 30, hatimaye jana Liverpool ilitangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England.

Liverpool imefanikiwa kubeba taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kupita miaka 30, huku ikiwa haipo uwanjani na kupitia runinga zao nyumbani, nyota wa Majogoo hao wa Liverpool walishuhudia Manchester City wakilambishwa mabao 2-1 na Chelsea kwenye Uwanja wa uwanjani Stamford Bridge na kuwapa nafasi hiyo ambayo waliisubiri kwa muda mrefu.

Kipigo hicho cha Man City kimethibitisha pengo la pointi 23 lililowekwa na Liverpool kileleni, haliwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo msimu huu, hivyo kufanya kikosi hicho cha Jurgen Klopp kutangaza ubingwa wakiwa na mechi saba mkononi.

Sasa, Man City waliokuwa mabingwa watetezi, watalazimika kujipanga kuwapa heshima yao Liverpool wakati watakapokutana kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu England.

Mechi 31, ushindi kwenye mechi 28, sare mbili na kichapo kimoja, kimetosha kuwapa Liverpool ubingwa. Kwa msimu huu, Liverpool imefunga mabao 70 na kufunga 21 tu, hilo likidhihirisha wazi huu ni mwaka mzuri kwao.

Kwa sasa Liverpool itacheza ikiwa haina presha yoyote huku ikiendelea na maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo ni mabingwa watetezi wa kombe hilo. Akiongea baada ya matokeo ya Chelsea na City juzi usiku, Kocha wa Liverpool, Klopp ambaye ndiye Kocha Mjerumani wa kwanza kutwaa taji hilo tangu michuano hiyo ianzishwe, alisema “Nimefarijika, nina furaha, najivunia, siwezi kuwa na furaha zaidi ya hii kwa vijana wangu.”