Lipuli yakomaa kwa Matola

Friday January 12 2018

 

By Matereka Jalilu

Dodoma. Viongozi wa Lipuli FC wamepinga tetesi kuwa kocha wao Suleiman Matola yuko mbioni kuachana na timu hiyo.

Taarifa za Matola kuondoka mjini Iringa zinatokana na kuwepo mvutano kati yake na viongozi wake wakati wa kikao cha kamati ya utendaji wa timu hiyo hivi karibuni huku ikielezwa kumekuwa na kutoelewana kwake na kocha mwenzake Amri Said.

Afisa habari wa Lipuli,Clement Sanga mbali na kukiri kutokuelewana kwa Matola kwenye kikao cha kamati ya utendaji ya timu hiyo, lakini kocha huyo hajavunja mkataba wake na timu hiyo.

“Siyo kweli kwamba Matola amekatishwa au kukatisha mkataba wake na timu yetu kama ilivyoelezwa na bado ni kocha halali wa timu yetu kwani bado ana mkataba nasi badala yake kulitokea kutokuelewana kwake na viongozi wakati wa kikao cha kamati ya utendaji,”alisema Sanga

Katika hatua nyingine kuhusu Matola kutajwa kutua Simba SC kuchukua jukumu la kocha msaidizi,Sanga alisema kocha huyo hafahamu taarifa hizo na endapo itakuwa hivyo atawasiliana na uongozi ili kujadiliana jinsi ya kulimaliza suala hilo.

Kwa mujibu wa Sanga, Matola yuko njiani leo Ijumaa  kuwahi mazoezi ya timu hiyo jioni tayari kwa mchezo wa kesho, Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo utakaochezwa Uwanja wa Samora mjini Iringa.