Lipuli mpo? Msiyempenda kaja

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Lusajo aliyewahi kukipiga Toto Africans na Yanga, alisema kwa sasa hakuna kulala na kila mchezo ni muhimu sana kwao katika kuiweka timu mazingira mazuri.

HAKUNA kulala. Ni neno alilotamka kinara wa mabao katika kikosi cha Namungo, Reliant Lusajo aliyeipeleka timu yake robo fainali ya Kombe la Shirikisho, huku akiitahadharisha Lipuli ijiandae kisaikolojia.

Lusajo aliyefunga mabao 10 mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara akimfuata kwa karibu kinara, Meddie Kagere wa Simba mwenye 14, ndiye aliyefunga bao la ushindi la Namungo wakati ikiiondosha Mbeya City ikiwa kwao jijini Mbeya kwa mabao 2-1 katika mechi ya Kombe la Shirikisho uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Sokoine.

Mara baada ya matokeo hayo, Namungo chini ya Kocha wake, Hitimana Thierry walijiandaa kusafiri kwenda Iringa kwa mchezo wao wa Ligi Kuu wikiendi hii dhidi ya ‘Wanapaluhengo’, Lipuli FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lusajo aliyewahi kukipiga Toto Africans na Yanga, alisema kwa sasa hakuna kulala na kila mchezo ni muhimu sana kwao katika kuiweka timu mazingira mazuri.

Alisema kila mchezo kwao ni vita ya kusaka ushindi, huku akibainisha kuwa kutokana na sapoti na ushirikiano walionao kikosini pamoja na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ndio siri ya mafanikio.

“Hatutaki masihara kabisa, tuko siriasi na mpira na tunashukuru tumefuzu Nane Bora ya Kombe la Shirikisho, kwa sasa tunaiwaza Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu ili kuendeleza ushindi,” alisema Lusajo mwenye digrii ya Biashara.

“Kwa mipango ya Mungu tutafikia malengo, kwani uwezo wa kubeba FA tunao, hayo mengine ya Ligi Kuu hatujui,” alisema Lusajo.