Lipuli hali tete

Muktasari:

Lipuli ni miongoni mwa timu ambazo zinapambana kukwepa rungu la kushuka Daraja, ambapo kwa matokeo ya leo yanaongeza presha zaidi kwa 'Wanapaluhengo' hao.

Mwanza. Lipuli FC imekubali kurudi mkoani Iringa ikiwa vichwa chini kufuatia vipigo mfululizo kutoka jijini Mwanza baada ya leo tena kubutuliwa mabao 2-0 dhidi ya Alliance FC.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili baada ya mechi iliyopita kulala kwa idadi hiyo ya mabao kutoka kwa Mbao FC na kushuka hadi nafasi ya 17 kwa pointi zao 37.

Katika mchezo wa leo licha ya kumiliki kwa asilimia kubwa mpira, lakini ishu ya kufanya maamuzi katika eneo la hatari kwa kufunga mabao iliwawia ngumu kwani michomo yao iliishia miguuni mwa mabeki wa Alliance.

Wenyeji walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza na dakika ya 34 David Richard aliweza kuipatia bao la kwanza akimalizia pasi safi ya Kiungo, Juma Nyangi na kuweza kuwapeleka mapumziko wakiwa mbele.

Kipindi cha pili Alliance walionekana kuutawala mchezo, licha ya Lipuli kupambana kudhibiti mashambulizi, lakini dakika ya 64, Vincent Samir aliweza kuongeza bao la pili akimalizia krosi ya David Richard na kuwachanganya kabisa wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo, Alliance wanafikisha pointi 40 na kuchumpa nafasi ya 14 baada ya kushuka uwanjani mara 34 na sasa mechi ijayo watakuwa ugenini kumenyana na JKT Tanzania.