Lionel Messi msimu huu anaitikisa dunia kimya kimya

Muktasari:

  • Tuzo ya sita ya mfungaji bora wa Ulaya Messi haongozi kwa kupachika mabao kwenye La Liga, bali pia ni kinara wa mabao wa ligi zote tano kubwa za bara Ulaya. Mpaka kufikia sasa, Messi amefunga mabao 26 ya La Liga, mabao tisa zaidi ya Luis Suarez, nane zaidi ya Kinara wa mabao wa EPL, Sergio Aguero (Man City).

WENGI walidhani kuondoka kwa Cristiano Ronaldo kwenye La Liga kutamaliza ufalme wa Lionel Messi kutokana na kumalizika kwa upinzani wao. Nani kakuambia? Messi hapoi. Msimu huu ndio kama amefunguliwa na mambo anayoyafanya hata kama humpendi, utamsikia tu.

Ulimwengu umeshuhudia vipaji vya kila aina vya soka. Pele, Maradona, Garrincha, Tostao, Rivaldo, Batistuta, Ronaldo de Lima, Zidane, Franz Beckenbauer, Antonio di Stefano, Johan Kruyff, Ronaldinho na wengineo wengi waliokuja na kutesa kwenye soka.

Katika soka la sasa, tumeshuhudia vipaji vingi tu kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Kylian Mbappe, Gareth Bale, Samuel Eto’o,

Didier Drogba, Eden Hazard, Vinicious Jr, Neymar na wengineo wengi. Lakini bila kumung’unya Lionel Messi ni ‘Genius’, ubora wake unafahamika. Anachoweza kukifanya uwanjani, hakihitaji maelezo.

Bila shaka, Murgentina huyu, ni mmoja wa wanasoka bora kabisa kuwahi kutokea katika sayari ya soka. Nani anabisha?

Hivi sasa anafikisha miaka 32, kwa kawaida katika umri huo, kwa mchezaji, kila mtu anategemea kiwango cha Messi kuanza kupungua. Lakini kwa wanaomfuatilia msimu huu, watagundua ‘Andunje’ amezidi kuwa mtamu.Kama ilivyo kwa mpinzani wake Cristiano Ronaldo, kadri anavyozidi

kuzeeka, ndivyo anavyozidi kuwa bora. Machi 9, Messi alifunga bao na asisti moja, katika ushindi wa 3-1, ambao Barcelona uliupata dhidi ya Rayo Valecano. Mahesabu yanasemaje?

Tuzo ya sita ya mfungaji bora wa Ulaya Messi haongozi kwa kupachika mabao kwenye La Liga, bali pia ni kinara wa mabao wa ligi zote tano kubwa za bara Ulaya. Mpaka kufikia sasa, Messi amefunga mabao 26 ya La Liga, mabao tisa zaidi ya Luis Suarez, nane zaidi ya Kinara wa mabao wa EPL, Sergio Aguero (Man City).

Messi ana mabao tisa zaidi ya kinara wa mabao kwenye Bundesliga, Robert Lewandowski, mabao saba zaidi ya Fabio Quagliarella na

Cristiano Ronaldo (Serie A), na mawili zaidi ya mpinzani wake mkuu katika mbio za kusaka ufalme wa mabao Ulaya, Kylian Mbappe (Ligue 1).

Bingwa wa kupika mabao Ulaya

Pamoja na kufunga mabao mengi zaidi ya kila mtu msimu huu, Messi pia ni mkali wa kupika mabao. Ni bingwa wa Asisti msimu huu.

Mpaka sasa amechangia kupatikana kwa mabao 12. Hakuna anayemfikia

kwenye EPL, Serie A, Ligue 1 na Bundesliga. Anayemkaribia ni Kiungo wa Chelsea, Eden Hazard, mwenye asisti 11.

Messi na Suarez, wanachuana na Real Madrid kufunga mabao Wakiwa wametoka kufunga bao moja kila mmoja katika ushindi wa 3-1,dhidi ya Rayo Valecano, Lionel Messi na pacha wake, Luis Suarez, ni kama wanashindana katika ufungaji na kikosi kizima cha Real Madrid.

Messi ana mabao 26, huku Suarez yeye akifikisha mabao 17, ambayo ni sawa na mabao 43, yaliyofungwa na Real Madrid, kwenye La Liga mpaka sasa.

Wakali hao wa kufumania nyavu, wameifanya Los Blancos, kuanzia kwa wachezaji hadi benchi la ufundi, wakose usingizi. Ukiangalia fomu ya Real Madrid, hasa baada ya Vinicious jr kuumia, ni ngumu kwao kuwapiku Messi na Suarez. Huu ni utani sasa!

Fundi wa kupiga ‘Free-kicks’

Messi alipofunga mabao mawili kwa ‘free-kick, dhidi ya Espanyol, mwezi Desemba mwaka jana, aliweka rekodi ya ufungaji wa mabao kwa mipira iliyokufa.

Hii ni rekodi mpya nchini Spain. Ilikuwa ni rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi, ndani ya msimu mmoja. Amefunga mabao 10 kwa njia hiyo. Ndani ya kipindi cha miaka mitano, Messi amekuwa moto wa kuotea mbali, katika upigaji wa ‘free-kick’. Achana na mbwembwe za Ronaldo. Messi anakukumbusha enzi za Ronaldinho na Beckham. Amefunga ‘free- kick nyingi zaidi ya Real Madrid, PSG, Bayern Munich na Liverpool.

Mchango wake ni mkubwa

Messi, amefunga asilimia 38 ya mabao ya Barcelona, msimu huu. Hiyo inamuweka katika nafasi ya pili kwenye La Liga, nyuma ya Christhian Stuani aliyefunga mabao 15 kati ya 27, zilizofungwa na Girona asilimia 56.

Ukijumlisha na Asisti zake, Messi anakuwa baba yao. Licha ya kufunga mabao mengi, Stuani bado anahaha kutafuta asisti yake ya kwanza. Messi amefunga au kuchangia kupatikana kwa mabao 38, kati ya 69 zilizofungwa na Barcelona. Kuna swali?

Hiyo ni sawa na ushiriki wa moja kwa moja, ambao ni sawa na asilimia 55 ya mabao yote ya Barcelona msimu huu. Hii sio mbaya sana, ikizingatiwa kuwa, ni PSG na Man City, tu ndio zilizofunga mabao mengi Ulaya.

Yupo kila mahali

Messi, sio kinara wa mabao na asisti kwenye La Liga pekee, anaongoza kila mahali. Kifupi Muargentina huyu, ameenea kila mahali. Ametoa pasi nyingi muhimu (pasi 3). Maana yake ni kwamba, kabla ya kila shuti, mguu wa Messi ulihusika kutoa pasi. Takwimu hazidanganyi.

Anaongoza kwa kupiga mashuti katika kila mechi. Ana wastani wa shuti 5.3, sawa na asilimia 33, amemzidi mkali wa mashuti wa Rayo Valecano, Raul De Thomas. Hata hivyo, msimu huu, hana takwimu nzuri ya kupiga chenga.

Anaweza kumaliza akiwa kinara wa vyenga, kwa kuangalia namna

anavyofanya katika kila mechi. Ana wastani wa chenga 3.9 kwa kila mechi.