Lionel Messi amsubiri Neymar arudi Nou Camp dirisha lijalo

Muktasari:

Nahodha huyo wa Barcelona amedai timu hiyo inamuhitaji Neymar kwa sababu ni mchezaji anayeweza kuipa mafanikio makubwa, huku pia akiwaomba mashabiki wampokee na kumsamehe kwa kitendo chake cha kutimkia PSG, mwaka 2017.

KAMA kuna kitu kitamfurahisha Lionel Messi wakati wa usajili wa majira ya kiangazi ni staa wa Paris Saint Germain, Neymar Jr kurudi Barcelona baada ya kutimkia Ufaransa miaka miwili na nusu iliyopita.

Messi amekiri angependa kumuona Neymar akirudi Barcelona kwa mara nyingine, huku akisisitiza Mbrazili huyo anajutia kuondoka Camp Nou na yuko tayari kuomba radhi kwa mashabiki wa timu hiyo.

Nahodha huyo wa Barcelona amedai timu hiyo inamuhitaji Neymar kwa sababu ni mchezaji anayeweza kuipa mafanikio makubwa, huku pia akiwaomba mashabiki wampokee na kumsamehe kwa kitendo chake cha kutimkia PSG, mwaka 2017.

Mbali na Neymar, Messi pia anatamani kumuona straika wa Inter Milan, Lautaro Martinez akitua Barcelona mwishoni mwa msimu huu kwa sababu anaamini staa huyo atatoa ushirikiano mzuri kwa Luis Suarez ambaye amekosa msaada katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona.