Lilian Internet: Amerudi kuwabamba tena

Muktasari:

Kitu kinachomfanya Internet kubamba zaidi basi ni staili yake ya kushusha masebene kwenye ngoma zake. Kwanza ana wanenguaji wa viwango kutokana na yeye mwenyewe kuifanya kazi hiyo kwa miaka 17 hivyo, hivyo shoo zake hazitakuwa za mchezo mchezo hata kidogo.

AGOSTI 27, 2016 Twanga Pepeta ilipiga shoo moja matata sana pale Mango Garden, Dar es Salaam. Shoo hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kumuaga mnenguaji aliyeikamata sekta hiyo kisawasawa. Ndio alikuwa Lilian Tungaraza a.k.a Lilian Internet, ambaye aliitumikia bendi hiyo kwa miaka 17.
Hata hivyo, wakati anatangaza kuachana na sekta hiyo ya mauno kila shabiki aliamini kwamba, Internet anakwenda zake kutulizana na kulea familia yake yenye watoto wawili kwa mumewe, Sheri.
Lakini, Internet alikuwa amewaza mbaali kuwa atarejea kivingine kabisa kwenye muziki na sasa ukiingia kwenye Youtube utakutana na ngoma za Wangu Moyo ambayo amempa shavu Barnaba, Nishawazima, Navimba, Together na Polepole ambazo ndio zimemtambulisha kwa mara nyingine tena kwenye game. 
Hata hivyo, Internet amechonga na Mwanaspoti na kufunguka mambo mbalimbali ikiwemo mipango yake ya kusonga mbele zaidi kwenye muziki.

KASI YAKE SASA
Achana na ngoma za Polepole, Together, Navimba na Moyo wangu ambazo zilimtambulisha vyema huku zikiwa na ladha ya Bongo Flava na dansi huku ndani yake Internet akikata mauno kama yote, kwa sasa anatamba na ngoma ya Mapenzi Mwimba.
Katika ngoma hiyo ya Mapenzi Mwimba ndani yake kuna sauti ya rapa aliyeiweka Twanga Pepeta kwenye ramani ya juu kabisa katika muziki wa dansi nchini, Msafiri Diouf, ambako ameshusha rapu za hatari sio mchezo.
Mbali na Diouf ambaye amechana kwelikweli, pia ndsani ya ngoma hiyo kuna mkono wa Miraji Shakashia na Jojo Jumanne ambao wamesimama kwenye gitaa.
“Wakati naingia kwenye game baada ya kustaafu kunengua, nilianza kwa kucheza kwenye anga za Bongo Flava, lakini kama unavyojua dansi iko ndani ya damu na sasa nimerejea huko n ahata ngoma zangu mpya utaona ni dansi tupu.
"Kwa sasa Mapenzi Mwiba ndio umebamba kinoma kwa sababu umepokewa vizuri na mashabiki wangu na hata wanamuziki waliotia mkono kwenye kolabo na kupiga vifaa ni matata kwelikweli,” anasema Lilian Internet ambaye enzi zake akipanda jukwaani kufanya yake usipomtunza basi utakuwa na sababu zako tu.

KOLABO NA MASTAA WA NJE
Ili uwe msanii mkubwa ni lazima ufanye kazi na watu wenye viwango vya kimataifa hivyo, nina mpango wa kufanya kolabo na wasanii wa nje ya Tanzania.
Lakini, Internet anasema kuwa kwa sasa yuko kwenye mchakato wa kukamilisha albamu yake ambayo ndani yake kuna mastaa kibao wa muziki wa dansi.

STAILI YAKE
Kama kuna kitu ambacho kitamfanya Internet kubamba zaidi basi ni staili yake ya kushusha masebene kwenye ngoma zake. Kwanza ana wanenguaji wa viwango kutokana na yeye mwenyewe kuifanya kazi hiyo kwa miaka 17 hivyo, hivyo shoo zake hazitakuwa za mchezo mchezo hata kidogo.
"Hapana, sitarudi kunengua lakini kwenye shoo zangu zote zitakuwa na sebene na nina wanenguaji wakali ambao watakuwa na kazi ya kuwapa mashabiki wangu burudani.
Lakini, sitawaacha hivi hivi kwa sababu bado nina mashabiki wengi, nitanengua kidogo kama kawaida,” anasema Internet.

TUJIKUMBUSHE
Miaka ya 200o ndio Lilian Internet alianza kuishika dansi wakati huo akiwa na bendi ya Diamond Sound wana Ikibinda Nkoi waliokuwa wakifanya yao pale Silent Inn, Mwenge.
Shoo ya Diamond haikuwa ikimalizika bila mashabiki kumuona Internet jukwaani huku akinogeshwa na rapa ya Allan Mulumba Kashama a.k.a Mstahiki Meya wa Jiji.
Baada ya kutamba sana na Diamond Sound, Lilian Internet akaibukia Twanga Pepeta na kwenda kukutana na wanenguaji wengine kama Rukia Bruno, Amina Rusha roho na Jessica Charles na Aisha Madinda.