Ligi Kuu ya KPL imerudi, Gor Mahia yachapwa Mombasa

Monday December 10 2018

 

By Eliya Solomon

UTAMU kunoga aiseeh. Ligi Kuu Kenya ‘SportPesa Premier’ imerejea kwa mabingwa watetezi, Gor Mahia kukiona cha moto mbele ya Bandari anayoichezea kiungo wa Kitanzania, Abdallah Hamis ‘Gattuso’.

Utepe umekatwa nchini Kenya kama ishara ya kuuanza msimu mpya wa SportPesa Premier Ligi kwa Gor Mahia ambayo imeachwa na Dylan Kerr kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji wao Bandari.

Gattuso wa Bongo hakuwa sehemu ya kikosi cha Bandari kilichoitandika Gor Mahia kutokana na majeraha aliyoyapata siku moja kabla ya mchezo huo. Kiungo huyo, anauguza ugoko baada ya kuchezewa vibaya mazoezini.

Hata hivyo, kwenye mchezo huo, alikuwepo kuhakikisha anatoa hamasa kwa wachezaji wenzake ambao walifanya kazi kubwa kuimaliza Gor Mahia yenye mastaa kama Humphrey Mieno Ochieng, Francis Kahata na Peter Fredrick Odhiambo.

Boda to boda ya Nje ya Bongo, imemnasa Hamis ambaye amefunguka kuhusu mchezo huo, namna ilivyokuwa hadi kuibuka na ushindi kwa mara ya pili mfululizo dhidi ya Gor Mahia.

Mwishoni mwa msimu uliopita Bandari ikiwa na Hamis ilivunja rekodi ya Gor Mahia ya kutopoteza mchezo hata mmoja kwa kukubali kipigo cha kwanza msimu huo wa 20117/18 cha mabao 2-1, Agosti 7 mwaka huu.

“Gemu ilikuwa ngumu lakini shauku yetu ya kuhitaji matokeo ilitusaidia, kuna muda mpira tuliumiliki kwa kiasi kikubwa ni kama tulikuwa tunapokezana maana na sisi tulikuwa tukimiliki.

“Umakini na nidhamu kwenye kushambulia ulitufanya kupata bao la kuongoza ndani ya dakika tatu za nyongeza, pia mwanzoni mwa kipindi cha pili tukapata la pili, wao walipata bao lao moja kwenye dakika ya 70,” anasema Hamis.

Mabao ya Bandari kwenye mchezo huo yalifungwa na mshambuliaji wa Kiganda, William Wadri na Mkenya, David Kingarua lile la kufutia machezo kwa Gor Mahia lilifungwa na Nicholas Kipkirui.

Michezo mingine ambayo ilipigwa siku hiyo ya ufunguzi wa Ligi ni Mathare United ambayo iliifunga Chemelil mabao 2-0, Homeboyz iliikaribisha KCB yenye Watanzania wengine, Jamal Mwambeleko na Peter Manyika JR kwa kipigo cha bao 1-0.

Posta Rangers ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Western Stima. SportPesa Premier Ligi iliendelea tena jana Jumapili kwa michezo kadhaa kupigwa.

Hamis mwenye majeraha ya ugoko alianza kucheza soka la mtaani Tarime, hapa anaeleza namna ilivyokuwa hadi kupata nafasi ya kucheza Kenya, haikuwa kazi nyepesi.

“Timu yangu ya kwanza kuichezea ilikuwa Tarime United na baada ya hiyo nikajiunga na Polisi Mara kwa mkataba wa miezi sita kisha nikaenda Stand United ambayo nilicheza na kuwa sehemu ya wachezaji ambao tulipambana na kuipandisha daraja.

“Nilicheza Stand United kwa makubaliano ya kunisomesha chuo maana kipindi hicho nilihitaji kujiendelea kwa kusomea inshu zinazohusu madini. Tulipomalizana niliamua kwenda Kenya kwa ajili ya kucheki upatikanaji wa ajira.

“Nilichopanga hakikwenda kama nilivyotaka na badala yake niligeukia tena soka kwa kutafuta timu ya kuichezea, nilihangaika sana na mwishowe nikapata ya daraja la kwanza,” anasema Abdallah.

Timu hiyo ya daraja la Kwanza Kenya ambayo alijiunga nayo Abdallah ni Muhoroni ambapo ilikuwa mwaka 2015 na akiwa timu hiyo kiungo huyo anasema alijipatia mafanikio ya kutwaa Kombe la Top 8 mbele Gor Mahia.

Hamis anasema alitwaa ubingwa wake wa kwanza Kenya akiwa kama nahodha wa Muhoroni na mara baada ya mashindano hayo alipata dili la kujiunga na Sony Sugar ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Kuu ya Kenya.

Mara baada ya kutua Sony Sugar, Abdallah anasema iliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

“Nikiwa Sony Sugar nilipata bahati ya kuitwa Taifa Stars na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki ikiwemo dhidi ya Botswana, Malawi, Benin na pia nilicheza machuano ya Cecafa pale Kenya japo matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wetu.

“Baada ya mashindano yale niliendelea kuichezea Sony Sugar huku nikijiwekea mikakati ya kutaka kuihama klabu hiyo ili nijiunge na timu kubwa zaidi ambayo itakuwa kwenye mbio za kuwania mataji,” anasema.

Abdallah anasema hakuwa na sababu za kujiuliza mbele ya ofa ya Bandari FC japokuwa awali Klabu ya AFC Leopards ndiyo iliyokuwa wa kwanza kuonyesha nia ya kumhitaji kuitumikia.

Advertisement