Ligi Ilemela imeanza kunoga Mwanza

Muktasari:

  • Ligi hiyo inashirikisha Klabu 12 ambazo zimegawanywa makundi mawili na kila kundi litatoa timu tatu kucheza hatua ya fainali ya kumpata Bingwa atakayepanda Daraja la tatu ngazi ya Mkoa.

 MWANZA. TIMU ya Jock Boys imepunguzwa kasi kwenye michuano ya Ligi Daraja la nne Wilaya ya Ilemela baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Buzuruga FC kwenye mchezo uliopigwa juzi katika uwanja wa Nyamagana.

Jock Boys ambao walishuka uwanjani wakiwa na rekodi ya ushindi wa mechi mbili mfululizo,walikumbana na kisiki mbele ya Buzuruga ambao waliweka ngumu kuhakikisha hawapotezi mchezo huo wa pili kwao.

Katika mtanange huo ambao ulionekana kuwa na ushindani kwa timu zote,Buzuruga ndio walitangulia kupata bao dakika ya 39 lililofungwa na Alex Dickson na kudumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana huku Buzuruga wakionekana kukosa nafasi za wazi na dakika ya 77 mabeki wa timu hiyo walijichanganya na kujikuta wakisawazishwa bao hilo kupitia kwa Amos Wayalla.

Kwa matokeo hayo Jock Boys wanafikisha pointi saba baada ya kucheza michezo mitatu,huku Buzuruga FC wakiweka kibindoni alama zao nne baada ya kushuka uwanjani mara mbili.

Kocha wa Buzuruga, Abeid Masoud alisema kuwa licha ya kujipanga kushinda mchezo huo lakini safu ya ushambuliaji ilikosa umakini na kushindwa kufunga mabao.

“Nitaenda kurekebisha makosa katika safu ya ushambuliaji ambao kiujumla wamekosa nafasi za wazi na leo tuliamini kwamba lazima tushinde,”alisema Masoud.

Kocha wa Jock Boys, Robert John alisema kuwa licha ya kukosa pointi tatu kwenye mchezo huo, lakini bado mbio za kuwania ubingwa zipo palepale na kwamba kikosi chake kina uwezo.