Ligi Hispania kurejea Juni 8

Muktasari:

Barcelona inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu ikiwa na pointi 58 na nyuma yake iko Real Madrid yenye pointi 56.

Madrid, Hispania. Baada ya kusimama kwa zaidi ya miezi miwili ikiwa ni hatua za kukabiliana na virusi vya Corona, Ligi Kuu ya Hispania imepewa ruhusa ya kuendelea tena kuanzia Juni 8 mwaka huu.

Serikali ya Hispania imetoa ruhusa kwa Bodi inayosimamia ligi hiyo (La Liga) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo (RFEF) kuendelea na shughuli za soka kuanzia tarehe hiyo baada ya kuwepo kwa unafuu kwa hali ya maambukizi ya Corona.

Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez amesema kuwa wakati umefika kwa masiaha ya kawaida kuanza kurejea nchini humu ikiwemo ligi za soka.

"Hispania imefanya kila linalohitajika na sasa anga jipya linafunguliwa kwa kila mmoja Muda umefika wa kurudisha shughuli zetu katika hali ya kawaida.

Kuanzia Juni 8, La Liga inaweza kurejea. Mpira wa Miguu una kundi kubwa la wafuasi lakini haitokuwa shughuli pekee ya burudani ambayo itarejea," alisema Sanchez.

Ingawa bado La Liga bado haijatangaza siku rasmi ya kurejea kwa ligi hiyo, inasemekana ilikuwa na matumaini kuwa mwanga wa ligi hiyo kurejea unaweza kuanza kuonekana kuanzia Juni 12.

Mwanzoni mwa wiki hii, klabu za Ligi Kuu Hispania zilipewa ruhusa ya kuanza mazoezi ya kujiweka sawa kwa ajili ya mtanange huo.

Hispania ni miongoni mwa nchi zilizopata madhara makubwa ya virusi vya Corona ambapo hadi leo, jumla ya mamba ya walioambukizwa ilikuwa ni watu 281,904, waliopona wakiwa ni 196,958 na idadi ya vifo ikiwa ni 28,628