Licha ya kipigo Simba yavuna mamilioni, Yanga yawangoja Ligi Kuu

Muktasari:

Kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi mitaani, Yanga walikuwa wakionekana kufurahia kipigo cha watani zao, huku wale wa Simba wakisisitiza ‘Tukutane TPL, tuone kama mtapata tiketi ya CAF’.

MASHABIKI wa Yanga jana Jumamosi walikuwa na furaha ya aina yake baada ya kushuhudia watani wao wa Simba wakinyooshwa mabao 4-1 ugenini na TP Mazembe na kung’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini fasta na wao wakajibu mapigo kwa kudai, Yanga wacheke lakini watakona katika Ligi Kuu.

Manazi wa Msimbazi wamedai hawajaumizwa sana na matokeo hayo, lakini kwa vile Yanga wamekejeli basi wanarudi nyumbani kuwaharibia katika Ligi Kuu Bara kwa kuhakikisha wanashinda mechi zao za viporo ili kuwatibulia Jangwani kuipa tiketi ya CAF kwa msimu ujao wa 2019-2020.

Kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi mitaani, Yanga walikuwa wakionekana kufurahia kipigo cha watani zao, huku wale wa Simba wakisisitiza ‘Tukutane TPL, tuone kama mtapata tiketi ya CAF’.

Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu wakiwa na alama 74 kutokana na mechi 31, wakati Simba ipo nafasi ya tatu na pointi zao 57 baada ya mechi 22 na kuwa na michezo 16 kabla ya kumaliza msimu ambayo kama itashinda yote itawafanya wamalize ligi wakitetea taji lao kwa mara ya pili mfululizo.

Ukiacha tambo hizo za watani, katika mchezo wa jana ambao Simba ilikuwa ikihitaji ushindi baada ya suluhu ya nyumbani na pia kutaka kulipa kisasi cha kufungwa mechi yao ya mwisho mjini Lubumbashi kwa mabao 3-1, Kocha Patrick Aussems aliwanzisha benchi Meddie Kagere na Clatous Chama kabla ya kuwaingiza kipindi cha pili na kujikuta wakilala tena ugenini kwa mara ya tano Afrika msimu huu.

Awali walicharaza 2-1 na Nkana Fc ya Zambia katika raundi ya kwanza, kisha kupoteza nyingine tatu mfululizo kwa AS Vita ya DR Congo kwa mabao 5-0, Al Ahly ya Misri (5-0) na JS Saoura ya Algeria waliowachapa 2-0.

Simba ilikumbana na kipigo hicho katika mechi yao ya marudiano ya robo fainali uliopigwa Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi na kuwaacha wababe hao wa mara tano wa Afrika wakitangulia nusu fainali ya michuano hiyo.

Wekundu wa Msimbazi walikuwa wa kwanza kuishtukiza Mazembe kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya pili tu ya mchezo kupitia Emmanuel Okwi akimalizia pasi mpenyezo ya Haruna Niyonzima, lakini wenyeji walicharuka na kuchomoa dakika ya 23 kupitia kwa Kabaso Chongo.

Uzembe wa mabeki Juuko Murshid na Zana Coulibaly ulimpa nafasi Elia Meschak kuiandikia Mazembe bao la pili dakika ya 38 mabao yaliyodu hadi mapumziko licha ya timu zote kushambuliaji kwa zamu.

Kipindi cha pili, Kocha Patrick Aussems aliwatoa kwa mpigo Juuko na Muzamir Yassin na kuwaingiza Kagere na Chama na kuifanya ngome ya Simba kuyumba na kuruhusu bao dakika ya 62 kupitia Tresor Mputu aliyewahi mpira uliokolewa vibaya na kipa Aishi Manula.

Wakati Simba ikijiuliza itarudishaje mabao hayo, ikajikuta ikitundikwa tena bao la nne dakika ya 75 ikitokana pia na uzembe wa mabeki, huku Manula akionyesha umahiri mkubwa wa kuokoa michomo ya nyota wa Mazembe ambao katika mchezo huo walipiga mashuti 34, huku 14 yakilenga lango.

Bao hilo liliwekwa kimiani na Jackson Muleka akitumia uzembe wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ hivyo kufikisha mabao matano katika mashindano hayo sawa na Mputu na Chama wa Simba.

Katika mchezo huo uliochezeshwa vizuri na mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia, Mazembe ilipata kona tisa, huku Simba ikipata tatu tu, huku Wekundu hao wakipiga mashuti matano tu, matatu yakilenga lango.

Wenyeji Mazembe wakimiliki mpira kwa asilimia 59 dhidi ya 41 za Wekundu wa Msimbazi, huku wakipiga pasi 425 dhidi ya 309 za Simba na pasi hizo kwa usahihi kwa wenyeji ulikuwa kwa asilimia 83 dhidi ya 78 za Msimbazi waliocheza faulo 12 dhidi ya 11 za Mazembe.

Timu zote ndani ya dakika 90 waliotea mara mbili na Simba ikipata kadi tatu za njano kupitia kwa Tshabalala, Juuko na Erasto Nyoni, huku wenyeji wakiwa hawaonyeshwa hata kadi moja.

YAVUNA MAMILIONI

Licha ya Simba kutolewa hatua hiyo ya robo fainali lakini imejihakikisha kuvuna mamilioni ya fedha kwani kutinga hatua hiyo kumewapa nafasi ya kuzawadiwa Dola za Kimarekani 650,000, huku straika wao Meddie Kagere akikwama kutimiza ndoto za kuwa Mfungaji Bora wa Afrika.

Kagere ameaga mashindano akiwa na mabao sita, akimuacha Moataz Al-Mehdi wa Al Nasr ya Libya mwenye saba akiwasikilizia kina Tresor Mputu na wenzake waliopo mashindanoni kama watakuja kumpita hadi kufikia tamati ya michuano hiyo Juni Mosi itakapopigwa fainali ya kutoa bingwa mpya.