Lewandowski hatajwi lakini noma!

Muktasari:

Mshambuliaji mahiri wa Poland, Robert Lewandowski, ni mmoja wa wapiga mabao mahiri kuwahi kutokea lakini hajawa gumzo Ulaya kama ilivyo kwa Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus, kutokana na sababu moja tu kucheza katika Ligi isiyo na mvuto, Bundesliga.

Munich, Ujerumani. Mshambuliaji mahiri wa Poland, Robert Lewandowski, hajawa gumzo Ulaya kama ilivyo kwa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, kwa sababu anacheza Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ ambayo haina mvuto kwa wengi.

Mshambuliaji huyo wiki iliyopita alifunga bao lake la 57 dakika ya 31 kabla ya kuongeza la 58 dakika ya 64 katika mchezo wake wa 100 wa michuano ya klabu barani Ulaya.

Mabao hayo mawili kwenye Uwanja wa Allianz Arena mbele ya mashabiki 70, 000, yaliipa Bayern Munich ushindi wa 2-0 dhidi ya AEK Athens ya Ugiriki na kuisogeza karibu na hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lewandowski,30, amekuwa mshambuliaji anayechomoza katika safu ya wafungaji bora wa ‘kila msimu tangu amejiunga na Borussia Dortmund mwaka 2010 alifunga mabao 74 katika mechi 131.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Munich mwaka 2014 ameifungia mabao 113 katika mechi 136, pia ameifungia nchi yake mabao 55 katika mechi 101 alizocheza.

Laiti angekuwa anacheza katika Ligi Kuu Hispania au England bila shaka Lewandowski angekuwa mshambuliaji gumzo duniani kutoka na umahiri wake wa kufunga.