Leon Bailey amfagilia Mbwana Samatta

Muktasari:

  • Winga wa Bayern Leverkusen ya nchini Ujerumani ameshindwa kuvumilia na kumwagia sifa mshambuliaji wa Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta. Samatta ambaye ni Mtanzania amekuwa akionyesha kiwango cha juu na kuwavutia mastaa mbalimbali wa Ulaya.

WINGA wa Bayern Leverkusen ya Ujeruman, Leon Bailey amempa tano nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwa kiwango anachoendelea kukionyesha Ubelgiji akiwa na KRC Genk.

Mjamaica, Bailey alisema Samatta amechangia kwa kiasi kikubwa KRC Genk kurejea kwenye Michuano ya Europa Ligi ambayo mara yao ya mwisho kushiriki ilikuwa msimu wa 2016/17.

“Samatta ni mchezaji hatari. Namkubali kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kufunga. Nimemuona kwa sasa yupo kwenye kiwango bora zaidi,” alisema winga huyo mwenye bao moja kwenye Bundesliga.

Bailey ambaye alicheza kikosi kimoja na Samatta msimu wa 2016/17 kabla ya kujiunga na Bayern Leverkusen, aliyasema hayo kupitia mtandao wake wa Instagram pindi alipokuwa Live.

Winga huyo kupitia mtandao wake alitoa nafasi kwa wafuasi wake kumuuliza chochote wanachojisikia ndipo Nje ya Bongo ilipotumia mwanya huo vizuri.

Hii ni mara ya pili, Nje ya Bongo kupata nafasi ya kuwasiliana na nyota ambao waliwahi kucheza KRC Genk na Samatta.

Nyota wa kwanza alikuwa Neeskens Kebano wa Fulham inayoshiriki Ligi Kuu England ‘EPL’ aliyetua nchini akiwa na Timu ya Taifa la DR Congo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars. Kebano alimfungukia Samatta kwa kusema hana maisha marefu Genk kutokana na utamaduni uliopo kwenye klabu hiyo wa kuwauza wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri.