Leicester City yairudisha rasmi Man United Uefa

Sunday July 26 2020

 

London, England. Kigogo Manchester United imefanikiwa rasmi kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Leicester City.

Matokeo hayo yanaifanya United kumaliza ligi ya England ikiwa nafasi ya tatu wakifikisha pointi 66 juu yao wakiwa Manchester City katika nafasi ya pili wenye pointi 81 mabingwa Liverpool wakiwa kinara wakiwa na pointi 99 huku Chelsea wakimaliza wanne wakiwa na pointi 66 wakitofautina na United mabao ya kufungwa na kufungwa.

United kupata ushindi huo walilazimika kusubiri mabao ya kipindi cha pili wakitangulia kuongoza kwa bao la mkwaju wa penalti ikifungwa na kiungo wao Bruno Fernandez dakika ya 71.

Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji Antony Martial kuangushwa katika eneo la hatari na mabeki wa Leicester City wakati akienda kumuona kipa Kesper Schmeichel.

Wakati Leicester wakitafuta bao la kusawazisha walijikuta wakifungwa bao la pili dakika za nyongeza likifungwa na Jesse Lingard aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Mason Greenwood akinufaika na makosa ya Schemeichel aliyekuwa akitaka kuondoa mpira katika eneo la hatari na mfungaji kuunasa na kufunga kirahisi.

Leicester hata hivyo dakika ya 90 walijikuta wakipata pigo la beki wao John Evans kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya kiungo Scott McTominay na kuipunguza kasi timu yake.

Advertisement

Advertisement